Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua yaitikisa Dar, vifo vyatajwa

Tue, 14 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Jiografia na mazingira ya Jiji la Dar es Salaam yameendelea kuwatesa wananchi wa jiji hilo, baada ya mvua zinazonyesha kusababisha madhara katika maeneo mbalimbali.

Taarifa za barabara kufungwa na vifo ni miongoni mwa madhara yaliyoripotiwa jana, na asilimia kubwa ya wananchi wanaotumia usafiri binafsi na ule wa umma kulazimika kutembea au kusota kwa saa kadhaa barabarani na vituoni wakisubiri usafiri kutokana na msongamano wa magari.

Watumiaji wa usafiri walikutana na changamoto ya kufungwa kwa maeneo ya barabara yaliyopitiwa na mabonde au mito na kushindwa kuendelea na safari kwa muda, au magari kupita kwa tabu kupitia njia za Kigogo, Msimbazi na Jangwani.

Katika baadhi ya barabara, foleni ya magari ilionekana kuwa kubwa, ikiwamo zile za Morogoro, Nyerere, Mandela, katikati ya jiji na Temeke.

Mwananchi lilishuhudia baadhi ya watu wakitumia usafiri wa bodaboda na mikokotoni kuwavusha katika baadhi ya maeneo ikiwamo Jangwani ili waweze kufika sehemu walizokuwa wakienda badala ya magari.

Mwananchi lilishuhudia magari yakishindwa kupita kipande cha barabara ya Magomeni Mapipa hadi Fire na kile cha Kigogo kupitia Jangwani yalipo makao makuu ya Klabu ya Yanga hadi Kariakoo.

Pia Soma

Kama njia ya kuepusha madhara, polisi walifunga baadhi ya barabara kuanzia saa 10:00 alfajiri, lakini ile ya Kawawa katika eneo la Mkwajuni (Kinondoni) magari madogo yalizuiwa kabisa kupita hadi maji yalipopungua. Kutokana na hali hiyo, mabasi yaendayo haraka (Udart), yalisitisha huduma za usafiri barabara ya Morogoro kupitia Jangwani na ile ya Kawawa kuelekea Morocco kutokana na maji mengi yaliyokuwa yakipita juu ya barabara hizo. Kwa barabara ya Kawawa maji yalijaa katika Bonde la Mkwajuni.

Aprili 8, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ilitabiri kuwa mvua kubwa itanyesha katika mikoa sita ikiwamo Dar es Salaam kabla ya utabiri mwingine unaoonyesha leo mvua kubwa itanyesha mkoani humo na ile ya Pwani, Tanga pamoja na visiwa vya Pemba na Unguja.

Watoto wafariki dunia

Kamanda wa polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema mvua hizo zimesababisha vifo vya watoto wawili katika maeneo tofauti.

Alisema Mei 8, mwili wa mtoto Francis Byabato (6) ulikutwa ukielea katika kisima kilichopo nyumbani kwao baada ya kupotea kwa siku mbili.

Mambosasa alisema tukio jingine ni la Mei 12, eneo la Mongo la Ndege ambako mwili wa mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 4-5 ulikutwa ukielea katika Mto Msimbazi. Mwili huo umehifadhiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Mambosasa alisema mvua hizo pia zimesababisha uharibifu mkubwa wa majengo ya shule za msingi Mwale na Majani ya Chai zilizopo Kiwalani pamoja na Sekondari ya Kibasila iliyopo Temeke, hali iliyosababisha kusitisha masomo kwa muda.

“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wakazi wa jiji hilo kuchukua tahadhari dhidi ya mvua hizo sambamba na kuwa makini na watoto wao,” alisema Mambosasa.

Mkurugenzi mtendaji wa Manispaa ya Ilala, Msongela Palela alisema kutokana na uharibifu wa shule watatenga bajeti kuzikarabati.

Alipoombwa kuzungumzia barabara zilizoharika jijini humo, meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa Dar es Salaam, Julius Ndyamukama hakuwa tayari kuzungumzia athari ya miundombinu kutokana na kuwa safari nje ya mkoa huo kikazi.

Mtendaji mkuu wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), Victor Seif hakupatikana kuzungumzia barabara zilizochimbika kutokana na mvua hizo.

Kutokana na msongamano wa magari unaosababishwa na barabara nyingi kuharibika, Mohamed Khatibu, mkazi wa Kariakoo aliitaka Serikali kuwa na utaratibu wa kujenga barabara imara ambazo haziwezi kuathiriwa na mvua za siku chache.

Chanzo: mwananchi.co.tz