Kilwa. Mvua zinazoendelea kunyesha wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi zimeharibu miundombinu ya shule za msingi Njinjo, Kisima Mkika, Ndende, Ruhatwe pamoja na kituo cha afya Njinjo.
Akizungumza leo Jumamosi Februari 15, 2020 mkurugenzi wa halmashauri ya Kilwa, Jofrey Jafari amesema kijiji cha Njinjo kimeathirika zaidi na mafuriko, wananchi wote wamehamishiwa kijiji cha Kipindimbi.
Amebainisha kuwa wanafunzi waliokuwa wakisoma katika shule ya Njinjo wameamishiwa katika shule nyingine zilizopo jirani.
"Shule ya msingi Njinjo tumeifunga kabisa na wanafunzi wote wamehamishwa. Halmashauri inaendelea kufanya marekebisho ya miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko hayo lakini shule. Tutatoa eneo jingine kwa ajili ya kujenga shule mpya,” amesema.
Amesema mvua hiyo imesababisha vyoo vya shule ya msingi, sekondari na zahanati kuharibika.
Amebainisha kuwa wananchi waliokumbwa na mafuriko wapo katika maeneo waliyopewa na Serikali kwa ajili ya kuanzisha makazi mapya na yale ya awali kuwa mashamba.