Mvua zinazoendelea kunyesha jijini Mbeya zimesababisha mafuriko yaliyobomoa makaburi ya jumuiya yaliyoko Kata ya Iganzo jijini hapa na kuacha baadhi ya miili ya watu waliozikwa katika makaburi hayo ikielea juu ya maji.
Tukio hilo lilitokea jana ambapo baadhi ya wakazi wa kata hiyo walilazimika kuanza kuhamisha miili ya ndugu zao na kwenda kuzika sehemu nyingine ambayo ni salama. Wakizungumza na wandishi wa habari wakati wa kuhamisha baadhi ya miili, wananchi hao walisema chanzo cha mafuriko hayo ni kukosekana mtaro imara kwenye eneo hilo, hali ambayo inasababisha maji kuanza kujitafutia njia makaburini.
Mmoja wa wananchi hao, Said Hasham alisema walimzika mama yao mwaka 2012 jirani na mtaro na hakujawahi kutokea tatizo lolote kwa zaidi ya miaka 10, ingawa wakati huo mtaro ulikuwa mdogo na hata maji yaliyokuwa yanapita yalikuwa kidogo na kwa sasa mtaro umepanuka kiasi kwamba umeanza kuathiri makaburi hayo.
“Kwa sasa maji ni mengi na yanazidi kupanua mfereji kiasi kwamba kwa sasa hata kuvuka hatuwezi, leo (jana) tumekuta kaburi la mama yetu limechimbika kiasi kwamba sanduku linaonekana kwa hiyo tumeamua kuhamisha ili tukazike sehemu nyingine,” alisema Hasham.