Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua yafukua makaburi miili yabaki nje

Mvua Yafukua Makaburi Mvua yafukua makaburi miili yabaki nje

Tue, 9 Apr 2024 Chanzo: Mwananchi

Taharuki na hofu vimetanda miongoni mwa wakazi wa Kata ya Iganzo jijini hapa kufuatia miili ya watu kufukuliwa na maji kwenye makaburi na kusombwa hadi kwenye makazi ya watu.

Kitendo hicho kimewafanya wakazi wa kata hiyo kuiomba Serikali iboreshe au kuyahamisha makaburi yaliyo karibu nao kwa sababu yanaweka rehani afya zao.

Mpaka sasa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, zaidi ya miili mitano imefukuliwa na maji karibu na mfereji uliopo kwenye makaburi hayo na mingine imesombwa na kukwama kwenye makazi ya watu.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Aprili 8, 2024, Ofisa Afya wa Jiji la Mbeya, Johnson Ndaro amekiri kuwapo na hali hiyo na ametahadharisha wananchi kuyaepuka maji yanayotiririka eneo hilo la makaburi ili wasiathirike kiafya.

Amesema licha ya kwamba mwenye mamlaka ya kuzungumzia kadhia hiyo yupo, lakini yeye kama mtaalamu wa afya ameshafika eneo la tukio na kutoa elimu kwa wananchi.

“Athari lazima ziwepo kwa sababu yale maji ni machafu kwa mazingira yanapotoka, kwa nafasi yangu nimeshafika pale makaburini na kuona hali ilivyo, tumekutana na wananchi wa maeneo yale na kuzungumza nao kuhusu madhara yatokanayo na maji hayo,” anasema Ndaro.

Mmoja wa wananchi wa kata hiyo, Queen Kalenga ameiambia Mwananchi kuwa; "tunaishi kwa hofu na mashaka makubwa, hatujazoea kuona miili ya watu waliokufa ikionekana hadharani, tunaomba Serikali ihamishe haya makaburi kwa sababu yapo kwenye mkondo wa maji,” amesema Kalenga.

Amesema maji ya mvua kufukua makaburi hayo hayajaanza katika msimu huu, bali ni hali ambayo ipo mara zote hasa mvua zikinyesha kwa wingi.

"Mimi binafsi nimeshuhudia miili zaidi ya mitano ikiopolewa, wikiwamo ya watoto wachanga. Tunaomba Serikali itusaidie afya zetu ziko hatarini,” amesema mkazi huyo.

Tumaini Samora, mkazi wa Mtaa wa Mkuyuni jirani na makaburi hayo amesema mvua zinaponyesha usiku wanakosa amani kwa kushuhudia miili au sanda zikining’inia kwenye makaburi, hali aliyosema inawaathiri kisaikolojia na familia zao, wakiwamo watoto.

"Kuna wakati wananchi tulichanga fedha kujenga mfereji, lakini nguvu zilikuwa ndogo tukakwama, hali ni mbaya makaburi mengine yako wazi, miili iko ndani na muda wowote mvua ikizidi tu itasombwa,” amesema Samora.

Mwanannchi limemtafuta Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, John Nchimbi azungumzia kadhia hiyo lakini simu yake imeita bila kupokewa na hata alipotumiwa ujumbe wa simu (SMS) haukujibiwa, lakini Meya wa Halmashauri ya Jiji, Dourmohamed Issa amekiri kuwapo kwa kadhia hiyo.

Amesema tayari wameanza mkakati wa kurekebisha m mfereji unaopita jirani na makaburi hayo ambao unaonekana kutiririsha maji mengi hadi eneo la makaburi.

“Lakini siwezi kujua mfereji huu unaoleta adha hii utafanyiwa kazi kwa muda gani, ila tunauandalia bajeti ili kuurekebisha baada ya shughuli ya kuyahamisha makaburi kushindikana,” amesema meya huyo.

Anasema “awali ilipangwa makaburi hayo yahamishwe, lakini kwa kuwa yako mengi, mpango huo umeshindikana badala yake tunataka kutenga bajeti ya kuukarabati mfereji unaopita makaburini hapo tumalize tatizo.

“Kumbuka haikuwapo bajeti hiyo, hivyo tunaenda kulichakata kwa sababu hatujafanya tathmini ili kubaini kiwango, lakini mkurugenzi naye ni mpya, hivyo tunalifanyia kazi,” amesema Meya Issa.

Watendaji wanena

Diwani wa Kata ya Iganzo, Daniel Mwanjoka amesema hali si nzuri kwa sababu licha ya jitihada zinazofanywa na wananchi kwa kushirikiana na Serikali za mtaa kuizika miili inayookotwa, kuna haja ya Serikali ya mkoa na viongozi wa dini hususan ya Kiislamu ambao waumini wa dini hiyo wamezikwa mahali hapo kuingilia kati sula hilo.

"Eneo hili la makaburi lilifungwa miaka 15 iliyopita kwa sababu yako kwenye eneo ambalo ni mkondo wa maji, yanasombwa kila wakati, lazima kifanyike kitu hapa ili yasiendelee kubomolewa na maji na wananchi tunusuru afya zao,” amesema diwani huyo.

Sheikh wa Mkoa wa Mbeya, Msafiri Njalambaha amesema changamoto hiyo walishaitolea taarifa mara kadhaa kwa halmashauri lakini hawajaona utekelezaji wake.

“Ni kweli changamoto hiyo ipo muda mrefu, tulishaifuatilia na kuitolea taarifa lakini hakuna utekelezaji, tunaomba nyie waandishi mtusaidie kufuatilia.”

“Lakini kuna kipindi ilielezwa kuwa itatengwa bajeti kwa ajili ya ukarabati hasa wa huu mfereji ili maji yasipande kwenye makaburi, ila bado hatujaona kama hilo limefanywa, amesema Sheikh Njalambaha.

Chanzo: Mwananchi