Dar es Salaam. Shughuli za kiuchumi na kijamii zimesimama jijini Dar es Salaam nchini Tanzania majira ya asubuhi leo Jumanne Desemba 17, 2019 kutokana na mvua zinazonyesha na kusababisha usumbufu kwa waendao kwa miguu na wenye magari.
Mbali na barabara kujaa maji baadhi ya mifereji nayo imefurika huku milio ya ngurumo za radi ikisikika huku anga likiwa katika hali ya giza.
Kando ya barabara baadhi ya watu wameonekana wakiwa wamejikunyata wakisubiri huenda mvua hii kubwa iliyoanza kunyesha ghafla mapema leo asubuhi itapungua ili waendelee na shughuli zao.
Hali hiyo ni mwendelezo wa mvua kubwa ambazo kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa angalizo kwa mvua kubwa kutokea kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Rukwa, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro.
Mwananchi limeshuhudia wakazi wa Tabata Kimanga wakikutana na adha baada ya daraja lililopo eneo la Chama kujaa maji hivyo kusababisha magari, bajaji na pikipiki kutopita na kuwalazimu watumiaji wa barabara hiyo kuvuka kwa kuyakanyaga maji hasa waendao kwa miguu.
Adha hiyo imegeuka fursa kwa wengine kwani walianza kuwabeba watu migongoni na kujipatia ujira wa Sh1,000 kwa kila mtu.
Eneo la Tabata Relini maji yamejaa kiasi cha kusimamisha shughuli za wafanyabiashara kama ilivyo Tabata Kisiwani ambako mkazi mmoja wa eneo hilo, Enock Kilumo alisema amefanikiwa kuvuka maji kwa shida ili tu awahi kazini.
"Dada huku sekta binafsi huwezi kujitetea mvua ndio maana nimevuka maji, kuna eneo nilitaka kusombwa ila wenzangu walinisaidia," amesema.
Mama ambaye alikua na mwanae, amesema uwingi wa maji hayo haukuzuia kuvuka kwa sababu alikua na watu wa kumsaidia.
Maji yamejaa katika barabara za ndaniĀ mitaa ya Tabata Segerea huku madaraja yakifunikwa kutokana na mvua hizo. Usalama katika barabara mbalimbali ni mzuri japokuwa kumekuwa na foleni kwa kipindi kifupi cha asubuhi.
Barabara ya Shekilango nako hali si shwari hasa eneo la Sinza Mugabe baada ya daraja kufunikwa na maji hali iliyosababisha magari kupitia njia ya Tandale. Ni hivyo hivyo eneo la Jangwani ambako maji yanapita juu ya daraja na kusababisha barabara hiyo kufungwa.