Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua ya mawe yaziacha familia bila makazi, yaharibu mazao

Wed, 13 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Geita. Mvua ya mawe iliyoambatana na upepo mkali imesababisha familia 10 katika kata ya Bulela halmashauri ya mji wa Geita kukosa mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kuezuliwa na upepo huku nyingine zikianguka.

Mbali na nyumba hizo pia eka zaidi ya 700 za mazao ya pamba, mahindi na mihogo zimeharibiwa na mvua hiyo pamoja na maghala mawili ya kuhifadhia pamba.

Wakizungumza na Mwananchi digtal, wananchi wa kijiji cha Nyaseke wamesema mvua hiyo iliyoanza kunyesha majira ya saa 11 jioni Machi 11 imewasababishia njaa kwa kuwa mazao yao yameharibikia shambani.

Ofisa mtendaji wa kijiji hicho, John Maguta amesema katika kijiji cha Nyaseke nyumba nne zimeharibika vibaya, ghala moja la pamba pamoja na eka zaidi ya 500 za mazao zimeharibiwa.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji wa Geita, Modest Apolnary amesema kwa sasa wananchi ambao nyumba zao zimeanguka wanaishi kwenye madarasa ya Shule ya Msingi Nyaseke wakati kamati ya maafa ikiangalia namna ya kuwasaidia.

Amesema uharibufu ni mkubwa hasa wa mazao na kwamba tayari kamati ya maafa imeanza ukaguzi ili kujua ukubwa wa tatizo.

“Imekua ngumu kujua uharibifu wa mazao ni mkubwa kiasi gani kwa kata nzima, bado maji ni mengi na njia hazipitiki tunaendelea kukusanya taarifa na timu yangu ya kilimo na ile ya maafa wapo huko wakikagua,’’ amesema Apolnary.

Scania Kahindi ambaye ni miongoni mwa familia zilizokosa makazi amesema mvua hiyo imeharibu kila kitu kilichokuwa ndani na kuomba Serikali na wasamaria wema wawasaidie ili waweze kujikimu kimaisha.



Chanzo: mwananchi.co.tz