Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua ya mawe yaharibu tumbaku ekari 250

45618 Pic+mvuaMvua ya mawe yaharibu tumbaku ekari 250

Sun, 10 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tabora. Mvua ya mawe iliyonyesha wilayani Sikonge, imeharibu zao la tumbaku na kukipa hasara kubwa Chama cha Msingi Kisinga.

Kaimu mkurugenzi mkuu wa bodi ya tumbaku nchini, Dk Julius Ningu, amesema leo kuwa mvua hiyo ilinyesha Machi 2 mwaka huu na kuharibu ekari 250.5 zinazolimwa na chama hicho cha msingi chenye wakulima 51.

Amesema hilo ni janga kubwa kwao kwa vile bahati mbaya hawana bima ya mazao ambayo ingeweza kuwafidia.

Amebainisha kwamba tathmini iliyofanywa ni kuwa kilo 136,669 zingepatikana kikiwa ni kiwango cha juu wakati hasara iliyopatikana ni Dola 213,534 ambazo wangezipata kama wangeuza baada ya mavuno.

Dk Ningu amesema ni wakati muafaka kwa wakulima kuhakikisha wanakuwa na bima ya mazao ili kuwaepusha na majanga kama hayo.

Ameeleza sasa wakulima wa chama hicho cha msingi wapo katika wakati mgumu kwa vile wana madeni waliyokopa benki ambayo yanatakiwa kulipwa. "Itabidi wavumiliwe walipe kwa misimu miwili hadi mitatu," amesema.

Chama hicho cha msingi hata hivyo kinatarajia kupata mavuno kidogo ambayo hayataweza kukidhi mahitaji na hivyo kukiacha na madeni ambayo itabidi yalipwe kwa awamu.

Chama cha msingi Kisanga ni mojawapo ya vyama vya msingi vinavyofanya vizuri wilayani Sikonge.



Chanzo: mwananchi.co.tz