Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua, uzito wa magari ya mizigo unavyoharibu barabara Mufindi

Mvua Mufindii.png Mvua, uzito wa magari ya mizigo unavyoharibu barabara Mufindi

Tue, 23 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mabasi ya abiria yanayofanya safari zake kwenye baadhi ya vijiji vya Wilaya ya Mufindi yamesitisha safari kutoka na ubovu wa barabara.

Uchunguzi umebaini mvua nyingi pamoja na magari ya mizigo yenye uzito mkubwa yanayotumia barabara hizo imekuwa chanzo cha kuharibika kiasi cha kutopitika.

Mabasi yaliyositisha huduma ni yale yanayofanya safari zake katika maeneo ya Usokame, Mapanda wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa pamoja na Mlimba Mkoa wa Morogoro.

Mufindi ni kati ya wilaya ambazo uchumi wake unategemea zaidi mazao ya misitu ikiwamo magogo, nguzo na mbao ambazo ili ziwafikie wanunuzi lazima malori yapakie na kupita kwenye barabara za vumbi.

Kulingana na Wakala wa Barabara Tanroads, Mkoa wa Iringa, uwezo wa barabara hizo ni kubeba tani 10 huku malori yanayotumia yakiwa ni tani 56 au zaidi.

Wakizungumza na Mwananchi Jana, Jumatatu Aprili 22,2024 baadhi ya madereva na makondakta wa magari hayo wamesema wamelazimika kusitisha safari.

Kondakta Anshon kaguo amesema ubovu wa barabara hasa kipindi hiki cha mvua imekuwa kero kubwa.

“Changamoto kubwa ni ubovu wa barabara wananchi wanasumbua lakini hatuna namna magari yapo gereji kama ambavyo mnaona yanaharibika kwa ajili ya ubovu wa barabara," amesema Kaguo.

Kwa upande wao, baadhi ya wasafiri wamesema hali ya barabara kwenye baadhi ya maeneo ni mbaya.

Wananchi hao, Emmanuel Kifanga, Lucia Sampeta, Jonthan kigodi pamoja na Jonason Haule walikuwa wakisubiri usafiri katika stendi ya mabasi ya Mafinga.

Kifanga amesema kutoka na hali hiyo wanalazimika kukodi pikipiki ambazo gharama zake ni zaidi ya Sh70,000 hadi Sh120,000 ikilinganishwa na basi ambalo hulipa kati ya Sh5,000 hadi Sh20,000 kwa mtu mmoja.

“Tunaiomba Serikali itusaidie kufanya marekebisho ya barabara katika maeneo mabovu ili tuweze kupata usafiri kwa gharama nafuu," amesema kifanga.

Jonathan kigodi amesema magari hayo yamesitisha huduma hiyo kutokana kero ya ubovu wa barabara zilizosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha.

“Maeneo ya Ugesa na kijiji cha Ukami miundombinu yake ni mibovu hivyo tuombe mamlaka husika kuangalia hususani barabara hizi zinazoenda vijijini kwa sababu zimekuwa na changamoto na zinaleta gharama kwa wananchi,” amesema.

Hali halisi

Baadhi ya wafanyabiashara wa mazao ya misitu wilayani Mufindi wanasema sio rahisi kutosafirisha mazao hayo kwenye barabara za vumbi.

"Ni kweli, hata wakitengeneza barabara tukipita tu na hii mvua zinaharibika. Tupite wapi sasa? Viwanda vipo mjini nasi lazima tupeleke malighafi huko," anasema Jolab Ngodi.

Amesema licha ya kuwa barabara hizo uwezo wake ni mdogo lakini kwa siku zaidi ya malori 30 hadi 50 yamekuwa yakipita.

Hatua za Serikali kunusuru barabara

Meneja wa Tanroads mkoani Iringa, Yudas Msangi amesema kutokana na mvua wakati mwingine hata mitambo ya wakandarasi inayoenda kufanya matengenezo, imekuwa ikifanya kazi kwa shida kwa kukwama na mingine ikianguka. Amekiri kuwa uzito wa magari na mvua nyingi zimekuwa zikiharibu barabara kwa kiwango kikubwa hivi sasa.

Mkakati wa ujenzi wa barabara za lami

Kulingana na Msangi, suluhisho la barabara hizo kwa sasa ni ujenzi wa kiwango cha lami ambao tayari Serikali imeanza kuchukua hatua.

Ametaja barabara zitakazojengwa kwa lami kuwa ni Nyololo - Mtwango, Mafinga - Mgololo na Igomaa - Kinyanambo A.

Mbunge wa Mufindi Kusini, David Kihenzile amesema baada ya mvua na uharibifu wa barabara alifanya ziara kuona hali halisi.

"Barabara ya Mafinga - Mgololo, mkandarasi amepatikana na yupo kwenye hatua za awali za ujenzi wa kiwango cha lami," amesema Kihenzile. Amesema eneo la Mtwango katika barabara ya Mafinga Mgololo ambalo lilikuwa linalalamikiwa limesharekebishwa.

"Barabara ya Nyololo – Mtwango lenye urefu wa kilomita 40 mkandarasi yupo kazini anajenga kwa kiwango cha lami," amesema Kihenzile.

Amesema barabara ya mji wa Igowole mkandarasi anatarajia kurejea baada ya kusimama kwa ajili ya mvua, huku barabara ya Sawala - Lulanda, ikiendelea na ujenzi wa kilomita 40 kwa kiwango cha lami.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live