Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua na upepo yasababisha watoto wawili kufariki, nyumba 16 kubomoka

43779 Ukelewepic Mvua na upepo yasababisha watoto wawili kufariki, nyumba 16 kubomoka

Tue, 26 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ukerewe. Watoto wawili wa familia moja wamefariki dunia huku watu 77 wakazi wa kijiji cha Mibungonanakwekwe wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza wakikosa makazi baada ya nyumba zao 16 kubomolewa kwa mvua iliyoambatana na upepo mkali.

Watoto waliokufa katika tukio hilo baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba walimokuwa wamelala wametambuliwa kuwa ni Nelson Benedictor (3) na Daison Benedictor mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Mulilo Jumanne Mulio amesema tukio hilo lilitokea jana saa 9:00 usiku wa kuamkia Februari 25.

Alisema watu wengine wa familia hiyo, Mektrida Benedictor (30) na Eric Benedictor (7) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu wa shule ya msingi Namakwekwe wamelazwa katika hospitali ya wilaya hiyo mjini Nansio kwa matibabu.

Mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Ukerewe, Dk Revocatus Cleophace alisema majeruhi katika tukio hilo wanaendelea vema na miili ya watoto waliopoteza maisha imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti hospitalini hapo.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kijiji cha Mabungonamakwekwe, Sabato Munubi hii ni mara ya pili kijiji hicho kukumbwa na kimbunga baada ya lile la mwaka 2000.

Mkuu wa wilaya ya Ukerewe, Colonel Magembe amesema kamati ya maafa ya wilaya inaendelea kufanya tathmini kujua madhara na msaada wa dharura unaohitajika huku akiwahakikishia waathirika Serikali itakuwa nao bega kwa bega katika kipindi hiki kigumu ikiwamo kuhakikisha wanapata chakula na gharama za misiba.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz