Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua kubwa Dar, barabara zajaa maji

Mvua Kuendelea Kunyesha Kwa Wiki Mbili | Mvua kubwa Dar, barabara zajaa maji

Fri, 8 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya kutulia kwa muda wa takribani majuma matatu, mvua kubwa inayesha jijini Dar es Salaam na kusababisha baadhi ya mito, mitaro na barabara kujaa maji.

Taarifa iliyotolewa jana Desemba 7, 2023 na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) inaonyesha uwapo wa mvua leo Desemba 8, 2023, huku hali ya bahari ikitarajiwa kuwa na mawimbi.

Mvua kwa baadhi ya maeneo ilianza jana jioni na kuendelea hadi leo Desemba 8, 2023.

Katika eneo la Kwa Sokota wilayani Temeke, maji yamefurika barabarani hali iliyosababishwa na mitaro kujaa maji.

Kutokana na hali hiyo, madereva wamekuwa wakitembea mwendo wa taratibu ili kuepusha uwezekano wa kutokea ajali.

Baadhi ya nyumba zilizopo eneo la Kwa Sokota zimeanza kuzingirwa maji hali iliyowalazimu wakazi wake kuyachota na kuyamwaga nje.

Katika barabara ya Morogoro maji yametuama barabarani na kutengeneza madimbwi katika baadhi ya maeneo hali inayowapa wakati mgumu watumiaji wa barabara hiyo.

Maeneo ambayo maji yametuama ni kituo cha mwendokasi cha Ubungo, Shekilango, Urafiki na Manzese ambayo kwa madereva wa vyombo vya moto wanalazimika kupunguza mwendo ili kupita maeneo hayo.

Madereva pia wanapita kwa tahadhari katika barabara hiyo kuanzia Kimara Korogwe hadi Ubungo, ambako baadhi ya maeneo maji yamejaa barabarani.

Baadhi ya waendesha bodaboda na bajaji wamejikuta wakirushiwa maji, baada ya kupishana na magari yaendayo haraka ambayo husababisha maji kurushwa.

Katika barabara ya Mandela, eneo kuanzia River Side hadi kwenye taa za kuongozea magari za External maji yamejaa barabarani, mitaro mikubwa iliyo pembezoni mwa barabara hiyo pia imefurika.

Baadhi ya wakazi wa maeneo ya Goba, Mbezi Juu na Ndumbwi imekuwa ngumu kwao kutoka nyumbani kutokana na jiografia ya maeneo hayo kuwa na milima na makorogo yenye tope kiasi ambacho usafiri wa haraka wa bodaboda haufanyi kazi.

Mkazi wa Ndumbwi, Sharifu Matiku amesema yeye ni fundi ujenzi na jana Desemba 7, 2023 walikubaliana na bosi wake awahi kazini kwa ajili ya ujezi lakini kwa hali ya mvua mpaka sasa 1.30 asubuhi ameshindwa kutoka nyumbani kuelekea Kijichi.

Mvua inaendelea kunyesha sasa ikiwa ni takribani wiki tatu baada ya iliyonyesha na kusababisha kufungwa kwa barabara ya Jangwani kutokana na kufurika maji kupita kiasi hali iliyofanya viongozi wa Serikali kuzuru eneo hilo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live