Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua Daraja la Dumila zaongeza kilomita 220 Dodoma - Morogoro

37128 Darajapic Dk Bashiru: Muswada huu usibadilishwe hata koma

Fri, 18 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Watu wanaosafiri kati ya Dodoma na Morogoro jana walilazimika kwenda kilomita 220 zaidi baada ya magari kuzuiwa kupita kutokana na maji ya mvua kujaa hadi juu ya daraja la Dumila lililopo mkoani Morogoro.

Kutokana na tatizo hilo, magari yote ya abiria yalielekezwa kutumia njia ya Melela – Mkata – Kimamba hadi Dumila ambayo inafanya kuwe na ongezeko hilo la umbali.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mkoa wa Morogoro, Doroth Mtenga alisema umbali wa barabara hiyo mbadala ni takriban kilomita 220. Safari ya Dar-Dodoma ni ya umbali wa zaidi ya kilomita 575.

Wakati magari mengine yakielekezwa kupitia njia hiyo ya muda, malori yalizuiwa na kutakiwa kusubiri kukamilika kwa matengenezo ya daraja hilo yaliyotarajiwa kukamilika jana jioni.

Kamanda wa polisi wa mkoa, Wilbroad Mutafungwa alisema japo hakuna madhara yoyote yaliyotokea zaidi ya kingo hizo kupata nyufa, wamezuia matumizi ya njia hiyo mpaka matengenezo yatakapofanyika.

Hii si mara ya kwanza kwa daraja hilo kukumbwa na mafuriko yaliyosababisha usafiri kati ya Dodoma na Morogoro uzuiwe kwa muda.

Mwaka 2014, mvua kubwa zilizonyesha mkoani hapa zilisababisha maji kupita kwa wingi juu ya daraja hilo na hivyo kuibua wasiwasi wa magari kusombwa au daraja kukatika.

Kutokana na hali hiyo, Januari 24, 2014 daraja hilo lilifanyiwa matengenezo. Aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, John Magufuli alilazimika kuweka kambi kwa siku tatu kusimamia matengenezo hayo.

Mtenga alisema tangu wiki iliyopita walibaini kuwapo kwa tatizo na kuweka mkandarasi ambaye tayari alishaanza kazi, lakini saa 9:00 usiku wa kuamkia jana, maji yaliongeza na kupita juu ya daraja.

“Mkandarasi yupo na tunachofanya ni kazi ya dharura ili kurejesha mawasiliano na magari yaweze kupita. Hapa tunajaza mawe ili kuweka uimara wa barabara. Tunaomba wananchi wawe wavumilivu,” alisema.

Mkuu wa mkoa, Dk Steven Kebwe alisema wataongeza nguvu ya wataalamu.

“Katika kuhakikisha daraja linarejea katika hali yake na kuanza kutumika, wahandisi wa Tanroads, wataalamu wanaotengeneza reli ya kisasa (SGR), kampuni inayotengeneza barabara ya Magole – Turiani – Rudewa – Kilosa na Mikumi wanashirikiana kutengeneza daraja hilo,” alisema.

Waliokwama

Abiria aliyekuwa akielekea Dodoma, Sauda Stambuli akiwa katika kituo cha mabasi cha Msamvu alifurahishwa na uamuzi wa kutumia njia mbadala na kuitaka Serikali kukarabati au kujenga upya Barabara ya Morogoro-Dodoma kutokana na umuhimu wake hasa baada ya Serikali kuhamishia makao makuu ya nchi huko.

Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Dumila, Jenifa Joseph anayeishi upande wa pili wa daraja hilo lililo katika Tarafa ya Magole alishindwa kuhudhuria masomo jana.

“Asubuhi nilifika hapa wakati naenda shuleni tukakatazwa na askari kuvuka kwa sababu ya usalama wetu,” alisema.

“Lakini pia tulitaka kuvuka kupitia kule chini (akionyesha sehemu ambayo watu walikuwa wakitumia kuvukia), lakini tukaona tuache kwa kuhofia kuchukuliwa na maji ambayo ni mengi,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz