Dar es Salaam. Mvua inayonyesha katika vipindi tofauti jijini Dar es Salaam imesababisha miundombinu ya soko la Mabibo maarufu ‘mahakama ya ndizi’ kuharibika na kusababisha usumbufu kwa wafanyabiashara na wanaofika sokoni hapo kununua bidhaa mbalimbali.
Kuanzia katika lango kuu la kuingilia soko hilo kuna matope hadi zilipopangwa bidhaa zinazouzwa kwa wateja.
Changamoto hiyo imekuwa fursa kwa baadhi ya vijana walioanzisha biashara ya kukodisha buti za mvua kwa wanaoingia kununua bidhaa.
Ukifika getini haraka vijana hao wanakuchangamkia na kukupatia buti hizo zinazokodishwa kwa Sh1,000.
Ukichana na ukodishaji wa buti huduma ya kuoshwa miguu inatolewa pia kwa wale ambao hawawezi kukodi viatu.
Elina Kingu ni mmoja wa watu waliokodi buti hizo baada ya kuona kwa viatu vyake asingeweza kukanyaga tope hilo.
Pia Soma
- Wapinzani Tanzania wahoji fedha za maendeleo ya kilimo kutolewa kidogo
- Mbunge CCM ataka wabunge kukatwa posho wapewe mawaziri, amtaja Lugola
- Afa akizungumza na simu iliyokuwa kwenye chaji
Meneja wa soko hilo Moses Olomi amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kueleza kuwa inatokana na asili ya eneo husika.
“Hapa tumeshaweka vifusi hadi basi, ni eneo lenye asili ya maji hivyo mvua zinaponyesha hali hii ni ya kawaida na hata wafanyabiashara wenyewe wameshazoea huwa wanajiandaa,” amesema Olomi.