Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mv Nyerere yanyanyuliwa baada ya kazi ya siku tano

19718 Kivuko+pic TanzaniaWeb

Sun, 30 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ukerewe. Wakati kivuko cha Mv Nyerere kikinyanyuliwa na kusimamishwa jana, biashara katika gulio la Bugorola imedorora.

Kivuko hicho kimenyanyuliwa na kuwekwa sawa ikiwa ni siku tano tangu kazi hiyo ilipoanza.

Kivuko hicho kilipinduka Septemba 20, mita 50 kabla ya kutia nanga katika gati la Kijiji cha Bwisya, kikiwa na zaidi ya abiria 250 waliokuwa wakitoka katika gulio la Bugorola wilayani Ukerewe kwenda Kisiwa cha Ukara

Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa ya Mv Nyerere, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema hadi jana mchana miili ya watu 228 ilikuwa imeopolewa huku watu 41 wakiokolewa wakiwa hai.

Kivuko hicho kimenyanyuliwa baada ya jitihada za siku tano, tangu Jumapili iliyopita ambako wataalamu wa uokoaji kutoka vyombo vya ulinzi na usalama wakiongozwa na maofisa wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wakishirikiana na makundi mbalimbali ya uokoaji wa ndani na nje ya Mkoa wa Mwanza.

Wataalamu hao wanaofanya kazi usiku na mchana walipitisha maboya maalumu chini ya maji yaliyojazwa upepo na kusaidia kukinyanyua juu kivuko hicho.

Pamoja na maboya, wataalamu hao pia walijaza maji ndani ya meli ya Mv Nyakibalya na kuyapunguza kidogo kidogo huku Mv Nyerere iliyofungwa kwa kamba kwenye meli hiyo nayo ikipanda juu ya maji.

Uokoaji wakamilika asilimia 85

Msimamizi mkuu wa shughuli hiyo, Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo alisema kazi hiyo imekamilika kwa asilimia 85 baada ya waokoaji na wataalamu kufanikiwa kukinyanyua na kusimamisha chombo hicho ambacho awali kilipinduka juu chini.

“Kazi kubwa iliyosalia baada ya kukinyanyua chombo sasa ni kutoa maji ndani, kukivutia nchi kavu na baadaye kukikagua kitaalamu kujua madhara kabla ya kuanza matengenezo,” alisema.

“ Kijeshi tunasema tunafanya re-organization. Kabla ya re-organization tunafanya uchunguzi kubaini kilichosalia eneo la tukio.”

Awali, Mabeyo pamoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa walitaka kazi ya kukinyanyua kivuko hicho ifanyike ndani ya siku tatu, lakini wataalamu mbalimbali wa uokoaji walisema ingechukua siku tano hadi wiki moja.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema kuanzia leo kivuko cha Mv Ukara ambacho awali kilikuwa hakitumiki, kimerekebishwa na kitaanza kufanya safari zake kati ya Ukara na Bugolora.

Gulio ladorora Bugolora

Hali ya biashara katika gulio la Bugolora katika Kisiwa Kikuu cha Ukerewe jana ilidorora kutokana na idadi ndogo ya wateja kutoka Kisiwa cha Ukara.

Mwandishi wa Mwananchi aliyekuwa mmoja wa wasafiri kutoka kisiwa cha Ukara kwenda kwenye gulio hilo alishuhudia idadi ndogo ya wafanyabiashara na wateja kulinganisha na siku zingine.

Gulio la Bugolora hufanyika mara moja kwa wiki kila Alhamisi. Bugolora ni kijiji cha mwisho kutoka Kisiwa cha Ukerewe kwenda Kisiwa cha Ukara. Wilaya ya Ukerewe ina visiwa vidogo 38 huku 34 wakiwa wanaishi wananchi.

Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Colnel Maghembe alisema Kisiwa cha Ukara chenye kata nne za Bwisya, Bukungu, Nyamagana na Bukiko kinakadiriwa kuwa na wakazi zaidi ya 50,000.

Mmoja wa wafanyabiasha katika gulio la Bugolora, Munyaga Marcel alitaja ajali kuwa sababu ya watu kuwa wachache. “Wateja wetu wengi wanatoka Ukara kwa sababu hawana gulio na mahitaji yao yote wanategemea kutoka gulio la Bugolora. Nadhani bado wako kwenye maombolezo ya vifo vya ndugu zao,” alisema Marcel.

Mfanyabiashara mwingine, Neema Mafuru anayeuza mbogamboga na matunda alisema mauzo yake jana yalishuka zaidi ya nusu kwa sababu wateja wake wengi ni wanawake wajasiriamali kutoka Ukara.

“Kuna wateja wangu wa uhakika zaidi ya 10 ambao nimepata taarifa ni kati ya waliokufa. Ni kilio cha msiba na biashara pia,” alisema Mafuru huku akifuta machozi.

Wakazi Ukara na gulio

Baadhi ya wakazi wa Kisiwa cha Ukara walisema licha ya hofu inayotokana na ajali ya kivuko, wataendelea kusafiri kwenda na kutoka gulio la Bugolora kwa sababu ndiko kunakopatikana mahitaji yote muhimu.

“Licha ya hofu inayotokana na ajali hii iliyotokea wakati wakazi wengi wa Ukara wakitoka kwenye gulio la Bugolora, bado tutaendelea kwenda gulioni kwa sababu ndiko tunakopata mahitaji kutokana Ukara kutokuwa na gulio,” alisema Msafiri John.

Kauli hiyo pia iliungwa mkono na Siwema Mariga aliyesema, “Nikiwa na fedha nitaenda gulio la Bugolora kwa sababu ndiko tunakopata mahitaji.”

Mkurugenzi halmashauri

Akizungumzia Ukara kutokuwa na gulio, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Ester Chaula alisema iwapo wananchi wa eneo hilo wataamua na kupitisha uamuzi wa kuanzisha gulio, halmashauri itashughulikia suala hilo kupitia vikao kwa mujibu wa kisheria, kanuni na taratibu.

“Suala hili ni jema lakini haliwezi kuamuliwa bila kupitia njia ya vikao halali vya halmashauri. Hata hivyo, suala hili linatakiwa kuanzia kwa wananchi kupitia vikao vyao vya kimaamuzi kuanzia ngazi ya vijiji na kata,” alisema Chaula

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alisisitiza ushirikishwaji wa wananchi katika suala la kuanzisha magulio katika maeneo yao.

“Kwenye hili (la kuanzisha gulio) wananchi na halmashauri za wilaya ndio wahusika wakuu. Sisi ngazi ya mkoa hili haliko kwetu ingawa hatutasita kushauri inapobidi au kuombwa,” alisema Mongella

Soma Zaidi:

·Mhandisi kivuko cha Mv Nyerere chini ya ulinzi

 

·Mv Ukara kuanza kutoa huduma badala ya Mv Nyerere

Chanzo: mwananchi.co.tz