Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muwango, DC aliyewekeza kwenye elimu

40323 Pic+muwango Muwango, DC aliyewekeza kwenye elimu

Wed, 6 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi, Rukia Muwango alifahamika zaidi wakati alipojitosa kuwatafuta watoto waliozaliwa na vichwa vikubwa na mgongo wazi kwa ajili ya matibabu.

Kampeni hiyo ilimfanya azunguke katika vyombo mbalimbali vya habari kuhamasisha wananchi wenye watoto hao wajitokeze ili wapate matibabu yaliyokuwa yanatolewa bure katika Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea, kwa msaada wa wataalamu kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI).

Mwenyewe anasema mafanikio ya kampeni hiyo ilikuwa ni kupona kwa watoto waliojitokeza kupata matibabu hayo.

Mwaka 2016, Muwango aliteuliwa kuwa mkuu wa wilaya hiyo akitoka kwenye nafasi ya ukurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa.

Anasema mkakati wake mkubwa ni kuhakikisha jamii ya Nachingwea inawekeza kwenye elimu akiamini kuwa hakuna changamoto itakayoshindwa kutatuliwa ikiwa wananchi wake watakuwa wameelimika.

Vipaumbele

Mkuu huyo wa wilaya anasema kipaumbele cha kwanza kwenye wilaya hiyo ni kuhakikisha kiwango cha elimu kinapanda kwa asilimia 100 kwa kuwa elimu ndiyo kila kitu.

“Wananchi wanaweza kuchangia maendeleo ya wilaya yao kama watakuwa na elimu ya kutosha. Tanzania ya viwanda inategemea elimu, hivyo, tunawekeza huko,” anaeleza.

Anasema kiuhalisia jamii iliyoelimika inaweza kupambana na changamoto nyingine za kimaisha ikiwamo afya, uchumi na mengine.

“Nikifumba macho yangu, naiona Nachingwea ya kesho yenye wananchi wenye amani na furaha, viwanda vilivyotelekezwa vimefufuliwa, wanawake na vijana wamepata ajira viwandani na wengine wamejiajiri na ufaulu wa wanafunzi umeongezeka,” anasema.

Mbali na elimu, DC huyo anasema kwa sasa hakuna wananchi wanaotembea mwendo mrefu kufuata vituo vya afya kutokana na huduma hiyo kusogezwa karibu.

Pia, anazungumzia kilimo: “Ninatamani kuona korosho ambayo ndiyo zao kuu la biashara linamkomboa kiuchumi mwana Nachingwea, na mengine mengi mazuri kama Ilani ya uchaguzi ya CCM inavyojieleza,” anasisitiza.

Kwa nafasi yake, Muwango ni mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM ya wilaya ya Nachingwea anakoingia kutoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM.

Wanafunzi wa kike

Muwango amesema mara nyingi amekuwa akipata muda wa kuzungumza na wanafunzi wa kike ili kuwapa moyo kwa kusoma kwa bidii waweze kutimiza ndoto zao.

“Changamoto kubwa inayowakabili ni kutembea mwendo mrefu kutoka shule kwenda nyumbani na kutoka nyumbani kwenda shuleni, hii inakatisha tamaa lakini huwa naongea nao,” anasema.

Anasema mkakati wao ni kuendelea kujenga mabweni ili wanafunzi wahamie shuleni.

Muwango anasema yapo mambo mengi yaliyofanyika wilayani humo tangu alipoteuliwa kushika nafasi hiyo.

“Najivunia kuona wazazi na walezi wamepata mwamko wa kupeleka watoto wao shuleni jambo lililokuwa linaniumiza sana kichwa tangu nilipofika kwenye wilaya hii,” anasema.

Anasema alichofanya ni kusimamia mahudhurio ya wanafunzi shuleni na kwamba uandikishaji wa madarasa ya awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza umeongezeka.

Chanzo: mwananchi.co.tz