Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mume, mke wajiua kwa kuuguza mtoto wao kwa muda mrefu

51231 KIFO+PIC

Wed, 10 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tabora. Kuuguza mtoto wao kwa muda mrefu inaelezwa kuwa ndiyo sababu ya wanandoa, Amina Juma na Kanuno Tano kujiua. Kwa mujibu wa Adam Kalonga ambaye ni babu wa Amina, mtoto Chiku Kudona (miezi tisa) amekuwa akiugua muda mrefu na kichwa chake kuongezeka ukubwa.

Kalonga alisema Amina alikatisha uhai wake kwa kunywa vidonge mchanganyiko vinavyotibu magonjwa ya binadamu.

Alisema Tano, ambaye ni mume wa Amina naye aliamua kujiua kwa kujinyonga mbali kidogo na nyumbani kwao baada ya mkewe kujiua.

Matukio hayo yote mawili ambayo kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Emmanuel Nley aliyazungumzia jana katika mkutano wake na wanahabari alisema yalifuatana.

“Mmoja wa watoto wa familia hiyo ameugua ugonjwa wa saratani kwa muda mrefu. Baada ya kumuuguza mtoto kwa muda mrefu mama aliamua kujiua,” alisema Nley.

Alisema baada ya taarifa za kifo cha mkewe kujulikana na mwili kuchukuliwa na polisi kwa uchunguzi, mumewe aliamua kujiua kwa kujinyonga akitumia pazia.

Kamanda Nley alisema matukio hayo mawili yameacha simanzi kwa familia, ndugu na majirani ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakishirikiana na wanandoa hao katika shughuli mbalimbali za kijamii.

Ndugu, jirani wazungumza

Akifafanua zaidi juu ya tukio hilo, babu wa Amina, Mzee Kalonga ambaye pia ni diwani wa Kata ya Kabila katika Manispaa ya Tabora alieleza kuwa kichwa cha mtoto wa mjukuu wake kilikuwa kikiongezeka kila uchao kiasi cha mama yake kujiua.

Alieleza kuwa mtoto huyo aliangushwa kwa bahati mbaya na mama yake wakati akipokezana na wifi yake miezi miwili iliyopita.

“Walikuwa wakipokezana mtoto, lakini kwa bahati mbaya aliwaponyoka na kuanguka chini na kuwa mwanzo wa matatizo ya kichwa chake,” alisema Kalonga.

Alisema wazazi walimpeleka mtoto huyo hospitali kwa ajili ya matibabu ikiwemo ya Kitete ambayo ni ya rufaa ya mkoa huo na Bugando, Mwanza ambako walipewa muda wa kurudi kwa ajili ya matibabu zaidi, lakini walishindwa kurudi Bugando kutokana na kushindwa kumudu gharama.

Kalonga alisema kabla ya tukio la mtoto huyo kuanguka, wanandoa hao walikuwa wanaishi vizuri kwa kipindi chote cha miaka mitano ya ndoa yao walichobahatika kupata watoto wawili - wa kwanza akiwa na umri wa miaka minne na wa pili ambaye ni huyo mgonjwa ambaye ana miezi tisa.

Mmoja wa majirani wa marehemu, Said Maulid alisema katika kipindi cha uhai wao wawili hao wamekuwa wakihangaika kumtibu mtoto wao huyo mdogo.

“Mama wa mtoto kwa kweli alikuwa akimhurumia mwanaye namna anavyoteseka na muda mwingi (mama) alikuwa akilia,” alisema Maulid.



Chanzo: mwananchi.co.tz