Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mume matatani kwa tuhuma za kumuua mkewe

Mauaji Mlll Mume matatani kwa tuhuma za kumuua mkewe

Thu, 5 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkazi wa kijiji cha Kakindo kilichopo Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera, Saimon Samson (30) anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za mauaji ya anayedaiwa kuwa mke wake, Merriness Jonathan (34), mkazi wa kijiji hicho baada ya mwili wake kukutwa umetelekezwa kwenye shimo la choo la shule ya awali.

Akizungumza leo Januari 05, 2022, mwenyekiti wa kijiji cha Kakindo, Paschal Bagaiga amesema mwili wa mwanamke huyo uligundulika ukiwa kwenye shimo la choo Januari 3, 2023 baada ya kupata taarifa kutoka kwa mwenyekiti wa kitongoji cha Mubembe kilichopo katika kijiji hicho, Nuru Amri kuwa kuna mtu ameonekana amenyoosha mkono juu kwenye shimo la choo ya wanafunzi wa awali katika kitongoji hicho.

Akisimulia tukio hilo Bagaiga amesema kuwa Desemba 28, 2022 alipokea taarifa kutoka kwa mjumbe wa Serikali ya Kijiji ambaye hakumtaja jina akimweleza kuhusu taarifa ya kupotea kwa Merriness ambaye alimweleza kuwa toka Desemba 21, 2022 majirani wanadai hawajamuona kwenye mazingira yake.

“Baada ya taarifa hiyo, nilitoa taarifa kwa polisi kata na kwa muda ule walimkamata mume wake, Saimon Samson (30) na rafiki wa marehemu, Mastidia Cosmas na kuwapeleka kituo cha polisi Bunaz na Mastidia alipelekwa polisi kwa tuhuma za kumhamisha mtoto wa marehemu wa darasa la tano na kumpeleka kwake na kusomba vitu vya marehemu na kuvipeleka kwake na baadaye rafiki wa marehemu alidhaminiwa.

“Katika mahojiano na polisi mume wa marehemu amedai kwamba alimsindikiza mke wake majira ya saa 3:00 usiku wakaagana, marehemu akaenda nyumbani kwake kulala ingawa Samson alitoa taarifa ya kupotea kwa mke wake kwa mwenyekiti wa kitongoji zikiwa zimepita siku nne toka mke wake amepotea,” amesema Bagaiga.

Amesema polisi walimtaka mwenyekiti wa kitongoji cha Mubembe lilipotokea tukio kuendelea na uchunguzi kumtafuta Merriness na Januari 3, 2023 majirani walianza kusikia harufu ya kitu kilichooza, ndipo waligundua mwili ambao umeshaanza kuharibika katika shimo la choo ya shule ya awali na kutoa taarifa polisi.

Ameongeza kwamba polisi walifika eneo la tukio wakiwa na mganga na baada ya kufanya uchunguzi wa mwili huo walibaini kuwa alikuwa ni mwanamke kwa kuwa waliona maziwa yake na hivyo wakagundua kuwa mwili huo ulikuwa ni wa Merriness na hivyo ukatolewa na kwenda kuzikwa.

Amesema marehemu alishafanyiwa jaribio la kuuawa mara mbili na huyo mume wake, mara ya kwanza alitaka kumnyonga wakiwa ndani, mtoto wa mwanamke huyo akapiga kelele, majirani wakafika na kuwasuruhisha na mara ya pili alitaka kumkata kwa panga akanusurika pia.

Shakiru Hamdan, shuhuda wa tukio hilo amesema Desemba 20, 2022, marehemu alikuwa na harusi ya binti yake na siku iliyofuata hakuonekana tena kwenye mazingira ya nyumba yake, ndipo walianza kumtafuta bila mafanikio na Januari 3, 2023 mwili wake ulipatikana kwenye shimo la choo cha shule ya awali, mita chache kutoka kwenye banda la mume wake alipokuwa anaishi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, William Mwampaghale amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema wanamshikilia mume wa marehemu, Saimon Samson ambaye siku ya Desemba 20, 2022 marehemu alienda nyumbani kwake na majira ya saa 3:00 usiku alimsindikiza wakaagana, mke akaenda kulala. Tangu hapo hakuonekana tena hadi mwili wake ulipokutwa kwenye shimo la choo.

Merriness ameacha watoto watatu na baba wa watoto hao alishafariki dunia na huyo anayetuhumiwa kusababisha kifo chake alikuwa hajazaa naye.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live