Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mume akimbia mke, kisa watoto hawa

Tue, 20 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Moja ya furaha katika ndoa ni kupata watoto. Lakini kwa Loveness Abdul (25), mkazi wa Wilaya ya Kasulu uzao wake wa watoto wawili uligeuka shubiri katika ndoa baada ya kutelekezwa na mumewe, Matokeo Hussein.

Kutelekezwa kwa mama huyo kulisababishwa na kilichodaiwa na mumewe kuwa ni kujifungua watoto wawili wenye tatizo la kutokuwa na sehemu ya haja kubwa.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu akiwa Hospitali ya Rufaa Bugando (BMC) jijini Mwanza alikofika kwa ajili ya matibabu ya mtoto wake, Loveness alisema tatizo la kujifungua watoto wenye matatizo kwenye njia ya haja kubwa lilianzia kwa mtoto wake wa kwanza aliyejifungua Januari, 2011.

Mkazi huyo wa Kigoma alisema licha ya kujifungua salama, mtoto wake huyo ambaye alifariki dunia Desemba 2012, alikuwa na tatizo la kutoa haja kubwa na ndogo kupitia sehemu moja ya haja ndogo licha ya kuonekana anazo njia zote mbili.

“Wataalamu waliokuwa wakimhudumia alipokuwa mkoani Kigoma, walisema njia yake ya haja kubwa ilikuwa imeziba. Alikuwa anapata maumivu makali wakati wa kujisaidia haja kubwa ambayo ilikuwa ikipitia njia ya haja ndogo,” alisema Loveness.

Tatizo hilo limejitokeza pia kwa mtoto wake wa pili, Hashiraf Hussein (mwaka mmoja na miezi miwili) ambaye yuko kwenye orodha ya watoto 25 wenye matatizo katika njia ya haja kubwa wanaosubiri kufanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando.

Timu ya wataalamu na madaktari bingwa kutoka Marekani wakishirikiana na wenzao wa Bugando walikuwa wamefanikiwa kuwafanyia upasuaji watoto 10 kati ya 25 walio chini ya miaka mitano watakaopata huduma hiyo ya bure kwa mujibu wa Sera ya Afya, huku wanaozidi umri huo wakichangia gharama.

Huku akibubujikwa machozi ya kukimbiwa na mume na fursa ya mtoto wake kutibiwa bure, Loveness alisema baada ya kujifungua mtoto wa pili mwenye tatizo kama hilo, mume wake alimkimbia.

“Siku moja kabla ya kuishia kusikojulikana hadi sasa, mume wangu aliniambia hawezi kuendelea kuishi na mwanamke anayezaa watoto wenye matatizo. Ni zaidi ya mwaka mmoja sasa nahangaika na mtoto wangu mwenyewe kumtafutia tiba,” alisema.

“Kabla ya kuja hapa Bugando, nilikuwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambako nilipewa rufaa ya kuja huku Bugando kuona kama Wazungu hawa (madaktari wa Marekani) watafanikiwa kumfanyia upasuaji. Niko hapa nasubiri nikiamini mtoto wangu atapona,” alisema.

Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Bugando, Dk Fabian Massaga alisema tayari timu ya wataalamu na mabingwa wanaoendelea na huduma ya upasuaji kwa watoto wenye tatizo la njia ya haja kubwa wamefanikiwa kuwafanyia upasuaji watoto kumi.

“Kwa waliozidi umri wa miaka mitano na waliofuata taratibu zote hadi kufika Bugando wanachangia Sh320, 000 kama gharama ya upasuaji huku watoto chini ya miaka mitano wakihudumiwa bure kwa mujibu wa Sera ya Afya,” alisema Dk Massaga.

Daktari bingwa wa upasuaji, ambaye pia ndiye mkuu wa kitengo cha upasuaji Bugando, Sista Alicia Massenga alisema upasuaji wa watoto hao 25 ungekamilika karibuni.

“Hospitali ya Bugando tayari imefanya upasuaji kwa watoto zaidi ya 100 wenye matatizo kwenye njia ya haja kubwa, wengine zaidi ya 200 wamefanyiwa uchunguzi wa kitaalamu,” alisema Dk Massenga.

Kiongozi wa wataalamu na madaktari bingwa kumi kutoka Marekani, Jason Frischer aliahidi kuwa wataendelea kushirikiana na Hospitali ya Bugando kuwahudumia watoto wenye uhitaji huku akiahidi kuwa wanaangalia uwezekano wa kufanya ziara ya kitabibu angalau mara mbili kwa mwaka. Sasa wanafanya ziara mara moja.

Ziara ya kitabibu ya wataalam na madaktari hao bingwa kutoka Marekani ilianza miaka minne iliyopita.



Chanzo: mwananchi.co.tz