Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mufti Uganda ashutumu polisi kuua, kupiga watu

13313 Pic+muft TanzaniaWeb

Thu, 23 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kampala, Uganda. Mufti wa Uganda Ramadhan Mubajje amevilaani vikosi vya usalama kwa kuhusika kuua na kuwapiga watu wakati wa uchaguzi mdogo na maandamano yaliyofanyika hivi karibuni.

Mubajje ambaye jana aliongoza sala ya Eid Al-Adha katika msikiti wa Old Kampala alisema vikosi vya usalama havikutumia weledi kuwapiga watu ambao walionekana kusalimu amri.

“Mtu amenyanyua juu mikono, kama ishara ya kujisalimisha au kutotenda kosa, lakini unakwenda unawapiga? Si jambo zuri. Watu kama hawa wanakuwa sababu za tawala kuchukiwa,” alisema Mufti Mubajje.

Ametoa wito watu kuheshimiana bila kujali itikadi za kidini au ufuasi wa kisiasa.

Kauli ya Mufti Mubajje imekuja katikati ya machungu ya watu kupigwa walipoandamana Jumatatu kupinga kushikiliwa kwa Mbunge wa Kyadondo Mashariki, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.

Maandamano hayo yalianza saa 4:00 asubuhi eneo la Kisekka Market na yalienea hadi barabara ya Kampala, Namirembe, Nakivubo Mews, Mtaa wa Ben Kiwanuka na Katwe ambako walitawanywa na vikosi vya usalama kwa mabomu ya machozi, fimbo na risasi za moto.

Umati wa watu ulikuwa ukiimba ‘Bobi Wine’ na maneno anayotumia sana ya; ‘Nguvu ya umma, Watu Wetu na Wakati ni Huu’.

Kamatakamata

Polisi wanawashikilia watu 103 waliokamatwa juzi na jana waliwakamata vijana watatu wa chama cha NRM, kwa kosa la kuandamana kushinikiza kutolewa kwa mbunge Bobi Wine.

Vijana hao wanaotoka Wilaya ya Kagadi walikamatwa wakijiandaa kuandamana jana huku wakiwa wameshikilia mabango ya kuitaka Serikali kumuachia mbunge huyo na mwenzake, Francis Zaake.

Mawakili wa Bobi Wine

Mawakili 24 maarufu wameungana kumtetea Bobi Wine, huku wakimtaka Mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu nchini Uganda, Med Kaggwa kuhakikisha anatumia vyema haki ya kikatiba ili kuhakikisha haki inatendeka.

“Kipindi hiki tunaamini kwamba Tume ya Haki za Binadamu ya Uganda itakuja na kauli kuhusiana na sakata hili. Tunatambua kuwa (Kaggwa) unayo mamlaka hayo,” amesema Erias Lukwago, mmoja wa wanasheria wa utetezi.

Kifungu cha sheria cha 53(2) cha katiba kinasema kwamba Tume inaweza kujiridhisha kwamba kuna uingiliaji wa haki za binadamu na uhuru (a) mtu aliyewekwa kizuizini (b) kuwapo kwa malipo ya fidia.

Katika mkutano wa Tume uliofanyika makao makuu mtaa wa Lumumba jijini Kampala, wanasheria hao wameibua hoja ya kuzuiwa kupatiwa matibabu, kupata usaidizi wa kisheria, kuzuiwa kuonana na familia pamoja na kuzungumza na waandishi wa habari kama makosa ya kuminya haki za utu.

Pia wamezungumzia polisi pamoja na maagizo kutoka mamlaka za juu kuzuia matumizi ya simu kwa watuhumiwa kuwasiliana na watu wengine.

Chanzo: mwananchi.co.tz