Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtwara yatajwa kiwango kikubwa watoto waliodumaa

10446 Mtwara+pic TanzaniaWeb

Sun, 1 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mtwara. Asilimia 38 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano katika Mkoa wa Mtwara wana udumavu uliotokana na kukosa lishe bora.

Hali hiyo imeleezwa kuchangia maendeleo duni ya watoto hao na kurudisha nyuma jitihada za Serikali pamoja na wadau wa maendeleo kupambana na jambo hilo.

Inaelezwa kuwa katika kila watoto 10, watatu wanakabiliwa na udumavu na kuufanya mkoa huo kuwa na idadi kubwa ya watoto wenye udumavu ikilinganishwa na kiwango cha kitaifa cha asilimia 34.

Hayo yameelezwa leo Jumamosi Juni 30, 2018 na Mkurugenzi  wa Elimu na Mafunzo ya Lishe nchini, Sikitu Saimon wakati wa utoaji  elimu kwa wahudumu wa afya ya jamii vijijini katika Wilaya ya Newala.

Amesema wamefika mkoani Mtwara kwa kuwa udumavu upo kwa kiwango kikubwa na wanachokifanya kwa sasa ni kutoa elimu.

“Tumeamua kutambua Mtwara kwa sababu, kwanza udumavu  uko juu ikilinganisha na ule wa kitaifa ambao ni asilimia 34,  pia hakukuwa na wadau wa masuala ya lishe,” amesema.

Meneja wa Mradi wa Utafiti unaolenga kupunguza tatizo la udumavu, Debora Niheya  amesema tatizo hilo halisababishwi na ukosefu wa chakula nchini, bali ni wa elimu.

“Tanzania sio sehemu ambayo hatuna vyakula vya kutosha au tuna shida sana kama ilivyo kwa baadhi ya nchi nyingine, lakini kuna shida kubwa sana tunaiona kwenye habari ya elimu na watu hawajui nini kifanyike,” amesema Niheya.

Kaimu Ofisa Utawala wa Wilaya ya Newala, Nadimu Mkanga amekiri wilaya hiyo kuwa na tatizo hilo na kusema katika vijiji 11 watoto 65 wametambuliwa kukabiliwa na tatizo hilo.

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz