Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtwara mbioni kukamilisha ujenzi wa madarasa

D7a8381c90c37c4d9e994b3f47190905.jpeg Mtwara mbioni kukamilisha ujenzi wa madarasa

Sun, 21 Nov 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mkoa wa Mtwara umeahidi kutangaza kukamilika kwa kazi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa Desemba 10 mwaka huu. Ujenzi huo unatekelezwa kupitia fedha za Mpango wa Maendeleo ya Taifa na Mapambano dhidi ya Covid-19 zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika fedha hizo, Mkoa wa Mtwara umepokea Sh bilioni 8.9 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 452 kwenye shule mbalimbali za sekondari mkoani humo.

Hayo yalibainishwa wakati Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Marco Gaguti alipofanya ziara ya kikazi kwenye baadhi ya shule za sekondari zilizopo Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Miongoni mwa shule alizotembelea ni Shule ya Sekondari ya Bandari pamoja na Mtwara Ufundi ambako alionesha kuridhishwa na kazi hiyo inavyofanyika. Katika fedha hizo, Manispaa ya Mtwara Mikindani imepokea Sh milioni 440 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 22 katika shule nane.

Shule ya Bandari ilipokea Sh milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne, Mtwara Ufundi ilipokea Sh milioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili. Nyingine zilizopo kwenye utekelezaji wa mpango huo katika manispaa hiyo ni pamoja na Shangani, Chuno, Mitengo, Mangamba, Sino na Naliendele.

Katika ziara hiyo, mkuu huyo wa mkoa alisisitiza na kuwataka viongozi wa mkoa huo kuhakikisha vifaa vinavyotumika katika ujenzi huo vinakuwa na ubora unaotakiwa kuwezesha kupata madarasa bora.

“Kila mtu ahakikishe kwamba vile viwango vinafikiwa vinginevyo ni hujuma kwa Taifa na ni muhimu kuwe na uchungu na wivu wa kuhakikisha kwamba miradi hiyo inafanyika kwa weledi, kwa ustadi na ubora unaostahili. Tusiruhusu mtu mmoja au wawili wakajinufaisha wakaweka maslahi yao mbele,” alisema Gaguti.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Said Mohamed alipongeza jitihada hizo za serikali kuona umuhimu mkubwa wa kuendelea kuboresha sekta ya elimu. “Hii yote ni kwa ajili ya kutuboreshea sisi wananchi tuweze kupata elimu bora na kwenye mazingira mazuri. Tunaunga mkono juhudi hizi na tanashiriki kikamilifu kwenye ujenzi huu,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz