Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtumbwi wazama Ziwa Victoria, wavuvi watatu wafariki

Picha Wavuvi Data Mtumbwi wazama Ziwa Victoria, wavuvi watatu wafariki

Tue, 9 May 2023 Chanzo: mwanachidigital

Wavuvi watatu wamefariki dunia huku wengine watatu wakinusurika baada ya mtumbi waliopanda kujaa maji na kuzama ndani ya Ziwa Victoria.

Waliopoteza maisha katika ajali hiyo iliyotokea jioni ya Mei 7, 2023, kwa mujibu wa Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Geita, Wambura Fidel wametambuliwa kuwa ni David Malyatabu (25), Kamuli Mhoja (20) na Faustine Cleofas (28), wote wakazi wa Kijiji cha Nungwe.

Akizungumza na wakazi wa kijiji cha Nungwe leo Mei 8, 2023 muda mfupi baada ya miili ya marehemu kuopolewa, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Cornel Magembe amewataka wavuvi kuchukua tahadhari kwa kusikiliza na kuzingatia maelekezo ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu hali ya hewa na upepo kabla ya kuingia ziwani.

“Pamoja na kuzingatia ushauri wa hali ya hewa, ni lazima vyombo vya uvuvi viwe na vifaa vya kujiokoa vikiwemo maboya na majaketi okozi kulingana na idadi ya wavuvi waliomo ndani ya chombo kama sheria inavyoelekeza,’’ amesema Magembe

Ameonya tabia na mazoea ya wavuvi kuingia ziwani bila vyombo vyao kuwa na vifaa okozi kwa sababu kufanya hivyo siyo tu ni uvunjifu wa sheria, bali pia ni kuhatarisha usalama wa vyombo na maisha yao.

“Waliofariki katika ajali hii ni vijana wadogo wenye umri chini ya miaka 30, familia na Taifa ilikuwa inawategemea. Serikali haiwezi kukubali kuona wananchi wanaendelea kupata madhara ambayo yangezuilika iwapo kila mtu atafanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria,’’ amesema mkuu huyo wa wilaya

Amewaagiza wamiliki wa vyombo vyote vya majini vikiwemo mitumbwi ya uvuvi wilayani Geita kuzingatia sheria na kanuni zinazoagiza kila chombo kuwa na vifaa okozi vikiwemo maboya na majaketi okozi kulingana na idadi ya waliopo kwenye chombo.

Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Geita, Wambura Fidel amewashauri wavuvi na wananchi kutoa taarifa za matukio ya ajali mapema kuwezesha shughuli za uokoaji kufanyika kwa wakati kunusuru mali na maisha ya watu.

‘’Kwa mfano, taarifa za ajali hii ya watu kuzama majini zimetolewa leo asubuhi ya Mei 8, 2023 wakati tukio limetokea jioni ya Mei 7, 2023,’’ amesema Wambura huku akiwataka wamiliki wa vyombo na wavuvi kuchunguza uimara na usalama wa vyombo vyao kabla ya kuingia ziwani.

Dixon Alphonce, mmoja wa wavuvi walionusurika katika ajali hiyo amesema mtumbwi wao ulijaa na kuzama maji wakati wakijitahidi kuokoa mtumbwi mwingine wa uvuvi uliokuwa umesogezwa na mawimbi ndani ya maji.

“Tulijtahidi kutumia vyombo kuchota maji na kuyamwaga nje lakini yalizidi na kuzamisha mtumbwi ndipo tukalazimika kujitosa majini kumbiga mbizi kujikoa huku tukipiga kelele kuomba msaada,’’ amesema

Chanzo: mwanachidigital