Kati ya watu 12 waliofariki katika ajali iliyotokea Kongwa mkoani Dodoma wapo askari wawili huku mtuhumiwa aliyekuwa akisafirishwa na mmoja wa askari akinusurika.
Ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia jana katika Kijiji cha Silwa kata ya Pandambili wilayani Kongwa mkoani Dodoma.
Ajali hiyo imetokea majira ya saa saba usiku ikihusisha lori lililokuwa limebeba Cementi lenye namba za usajili T677 DVX na basi la kampuni ya Frester lenye namba za usajili T 415 DPP lilokuwa likitoka Bukoba kwenda Jijini Dar es salaam.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Alhamisi Februari 9,2023,Kamishana wa Operation na Mafunzo Jeshi la Polisi Tanzania, Awadh Haji amesema katika ajali hiyo kulikuwa na mtuhimiwa aliyekuwa akitokea Mwanza na alikuwa akipelekwa Jijini Dar es salaam.
Amesema kwa bahati mbaya askari ajulikanaye kwa jina la Coplo Hamis aliyekuwa akimsindikiza amefariki huku mtuhumiwa akipata majeruhi na wanaendelea kumshikilia.
“Mtuhumiwa amepona tupo nae yupo chini ya ulinzi, bahati mbaya tumempoteza askari,”amesema Kamishna huyo.
Kamishana huyo amesema pia amefariki askari mwingine (bila kumtaja jina) aliyekuwa akienda masomoni katika chuo cha upolisi Kidatu mkoani Morogoro.
“Alikuwa akitokea Tabora kwenda Chuo cha Kidatu kuhudhuria mafunzo ya cheo ni habati mbaya tumempoteza,”amesema Kamishana huyo.