Dar es Salaam. Mtoto Shaaban Ngunda, mwenye umri wa miezi sita amepotea katika mazingira tatanishi eneo la Mbagala Charambe wilayani Temeke baada ya kuchukuliwa na mtu ambaye bado hajajulikana. Akisimulia jana namna mwanaye alivyopotea, Mama mzazi wa Shaaban, Binati Nongwa alisema tukio hilo lilitokea Novemba 6. Siku ya tukio anasema alikwenda kumtembelea aliyekuwa jirani yake aliyemtaja kwa jina la Mama Rose anayeishi mtaa wa Ubungo, Charambe aliyemuita akamtembelee. Mama huyo ambaye alikuwa akisimulia mkasa huo huku akilengwa na machozi, alisema alianza safari ya kwenda huko saa sita mchana akiwa na mwanaye mgongoni. “Nilipofika nilimkuta amekaa na wanawake wengine, siwakumbuki idadi yao. Niliwasalimia na kukaa chini, nikamwambia Mama Rose nina njaa, akaniambia nimshushe mtoto chini niende nikanunue samaki tuje tusonge ugali, akanipatia Sh1,000. “Niliinuka na kumuacha mwanangu akiwa amepakatwa na mama Rose, lakini baada ya kurudi sikumuona mwanangu, nikamuuliza yuko wapi, akasema hajui alipo,” alisimulia Binati ambaye ana watoto watano. Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa mtoto huyo kutoonekana hadi jana. Hata hivyo, Mwananchi lilitaka kufahamu kwa kina mkasa huo, likamtafuta Mama Rose kusudi azungumzie sakata hilo, likaambiwa anashikiliwa na Polisi. Mwananchi lilifanikiwa kuzungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, Emmanuel Lukula ambaye alikiri kuwapo kwa tukio hilo ambalo alisema wanaendelea kulichunguza. Awali, ilielezwa kuwa tukio la kupotea kwa mtoto huyo liliripotiwa katika Kituo cha Polisi Maturubai, eneo la Mbagala Charambe, lakini likahamishiwa kituo cha Polisi Chang’ombe. “Ni kweli kuna cheating (udanganyifu) umefanyika jinsi mtoto alivyochukuliwa. Polisi imeshaanza uchunguzi. “Ila ninavyofahamu kesi hii ipo kituo cha polisi Maturubai Mbagala. Lakini nashangaa unavyoniambia imehamishiwa Chang’ombe. Kwa sababu kituo cha Maturubai kina hadhi sawa na hiki kwanini kesi hiyo iletwe huku? ila nitafuatilia kujua nini kimetokea hadi ihamishiwe hapa,” alisema Kamanda Lukula. Akijifuta machozi mara kwa mara wakati akisimulia mkasa wa kuibiwa kwa mwanawe, Binati alisema alipombana zaidi mama Rose amweleze mwanawe yuko wapi, akamwambia atoke nje akamuangalie nje kama yuko. “Nilishindwa kumuelewa anasema nini, kwa sababu nilipofika pale nilikuwa na mtoto wangu na nilipoondoka nilimuachia yeye akiwa kampakata, halafu namuuliza ananijibu vitu visivyoeleweka,” alisimulia mama huyo. Akisimulia tukio lilivyokuwa, mama mdogo wa Shabaan, Siri Nongwa alidai Novemba 5 saa tisa alasiri akiwa nyumbani kwao Mtaa wa Mponda, alimtuma mtoto mkubwa wa Binati, Said Ally (13) akamnunulie bidhaa kwa ajili ya biashara zake. Lakini njiani alikutana na mama Rose aliyemwagiza akamwambie mama yake (Binati) anamuomba aende nyumbani kwake ana mazungumzo naye. “Mama Rose na dada yangu ni mtu na rafiki yake, kwa sababu walikuwa wanaishi wote Mtaa wa Ubungo,” alisema Siri. Alisema baada ya Said kurudi nyumbani, alimfikishia ujumbe mama yake huku akimsisitiza kuwa ameambiwa asikose kwenda. “Nilimuuliza Said kuna nini, mbona Mama Rose amesisitiza hivyo. Hata hivyo sikuwa na wasiwasi kwa sababu ni marafiki na walikuwa majirani,” alisema Siri. Hata hivyo, Siri alisema ingawa polisi wanamshikilia Mama Rose, aliwaomba waongeze nguvu katika uchunguzi ili kuhakikisha mtoto huyo anapatikana kwa kile alichodai familia ipo kwenye wakati mgumu. Kwa mujibu wa Siri, alidai siku za nyuma walipata taarifa kutoka kwa majirani wa Mtaa wa Mponda kuwa kuna watu walimfuata dada yake na kumtaka awauzie mtoto, lakini alikataa. Naye Bibi yake Shabaan, Rukia Mbwana alisema wakati mwanaye anapatiwa taarifa ya wito, alikuwa na ndugu zake zaidi ya watano akiwamo mumewe Binati. “Nilimuuliza Said huu wito una heri mbona umekuwa una msisitizo, akanijibu hajui, lakini sikuwa na shaka,” alisimulia Rukia. Kwa mujibu wa Rukia, siku hiyo ilipotimu saa 12 jioni alipata taarifa kutoka kwa majirani kuwa mjukuu wake amepotea katika mazingira ya kutatanisha. “Sikula chakula siku hiyo, nilijisikia uchungu, nikaanza kukumbuka ule wito wa msisitizo ndiyo nikazidi kuchanganyikiwa, sijui yuko wapi maana tumemtafuta sana. “Tunaomba polisi watusaidie, tumeshatoa taarifa kwao na wametuahidi wanafanya uchunguzi, lakini muda unakwenda hatuoni dalili. Tumefika hadi Mkuranga na Kibiti kumtafuta baada ya kusikia kwenye taarifa ya habari kuna mtoto mdogo ameokotwa,” alisema. Aliongeza kuwa kwa sasa familia ipo katika majonzi na hakuna kinachofanyika zaidi ya kuamka asubuhi kumuomba Mungu kisha kuhangaika huku na kule kumtafuta Shabaan. “Tupo katika wakati mgumu sana.Tumekuwa watu wa kulia na kubembelezena kila siku, polisi itusaidie kumpata mtoto huyu,” alieleza. Kwa upande wake, Babu yake Shabaan, Issa Nongwa alisema: “Naomba polisi itusaidie maana tumemtafuta sana mjukuu wetu bila mafanikio.