Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtoto wa Rais apinga nyumba kubomolewa

Balozi Ali Karume Balozi Ali Karume.

Thu, 6 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mtoto wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Balozi Ali Karume amepinga kuvunjwa kwa nyumba za Maendeleo Kilimani mpango ambao amesema unakwenda kinyume cha uamuzi uliopitishwa na Baraza la Mapinduzi kwamba nyumba hizo zifanyiwe matengenezo ili kulinda historia yake.

Balozi Karume aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake, Maisara, Mjini Unguja, kuhusu kumbukumbu ya miaka 51 ya kifo cha Hayati Abeid Amani Karume inayofanyika Aprili 7, kila mwaka.

Alisema kwa mujibu wa sheria na katiba, ardhi ni mali ya serikali lakini serikali inaweza kuchukua ardhi ya mwananchi iwapo katika eneo hilo kunajengwa mradi wa maendeleo wa huduma za jamii na wananchi lazima walipwe fidia na si mradi wa biashara.

Pia alisema kama wananchi wa Kilimani hawataki nyumba zao zivunjwe wanapaswa kupeleka msimamo wao serikalini na si kulalamika mitaani kwa sababu wana haki kwa mujibu wa Katiba na sheria ya kukataa mradi huo.

“Baraza la Mapinduzi chini ya Rais mstaafu Dk. Ali Mohamed Shein, lilipitisha uamuzi kuwa nyumba za Kilimani zifanyiwe matengenezo makubwa na si kuvunjwa baada ya kukumbwa na uchakavu,” alisema Balozi Karume.

Alisema bahati mbaya kwa wakati huo serikali haikuwa na fedha za kufanyia matengenezo nyumba hizo, lakini uamuzi huo uliendelea kubaki na kuwa mpango wa siku za baadaye katika kulinda nyumba za maendeleo zilizojengwa na Rais wa Kwanza wa Zanzibar baada ya Mapinduzi ya Januari 12. 1964.

“Katika nyumba hizo mama angu alipata fleti moja na mimi nikapokea taarifa kupitia jirani yetu akaniambia nyumba za Kilimani umesikia zinavunjwa kupisha mradi wa uwekezaji wa nyumba za kisasa lakini hatujui tutahamishiwa wapi?” alihoji Balozi Karume.

Aidha, alisema Baraza la Mapinduzi ndilo lenye uwezo wa kufuta uamuzi wake lakini inashangaza serikali imeamua kuvunja nyumba za kilimani, ili kumpisha mwekezaji ajenge nyumba za makazi ya biashara.

Balozi Karume alisema wakati wa utawala wa Dk Shein, yeye akiwa Waziri wa Ujenzi, Miundombinu na Mawasiliano, alimwagiza kufanya ziara katika nyumba za Kilimani baada ya kupokea malalamiko kuwa nyumba hizo zinakabiliwa na uchakavu na baadhi ya wakaazi wake wanatumia kuni kwa ajili ya kupikia na kusababisha uharibifu zaidi.

“Nilipofanya ukaguzi katika nyumba hizo tuliandika ripoti na kupeleka kwa rais na baadaye suala hilo lilijadiliwa baraza la mapinduzi na kufikia maamuzi nyumba hizo zianze kufanyiwa matengenezo ili kulinda historia yake,” alisema Balozi Karume.

Alisema katika nyumba 406, serikali kupitia Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC) wana nyumba 14 na zilizobakia ni mali ya wananchi ambao walipewa kama fidia kupisha mradi wa ujenzi wa nyumba hizo.

Alisema nyumba hizo zimejengwa na rais wa kwanza baada ya mapinduzi januari 1964 ukiwa ni msaada kutoka serikali ya Ujerumani na kila mwananchi ambae nyumba yake ilivunjwa katika eneo hilo alifidiwa nyumba moja kwa ajili ya makazi.

Katibu wa Kamati Maalum, Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Khamis Mbeto, alisema wananchi wa Kilimani ndio waliomuomba Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi kuzifanyia matengenezo nyumba hizo kwa madai zinakabiliwa na uchakavu.

“Rais Dk. Mwinyi alifanya ziara ya kuwatembelea wagonjwa katika eneo hilo lakini alipokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa eneo hilo kuwa nyumba hizo zimekabiliwa na uchakavu kabla ya kuja na mradi wa kujenga nyumba mpya na wanaoishi katika nyumba hizo kupisha ujenzi kwa muda na baada kumalizika kukabidhiwa nyumba zao,” alisema Mbeto.

“Kama wananchi hawataki kuhama nyumba hizo zitakapokuja kubomoka wasije kuilaumu serikali kwa sababu nia ya serikali ni kuvunja nyumba hizo na kujenga zingine chini ya mradi wa Mwinyi City,” alisema.

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara wa kujadili ujenzi wa nyumba hizo, walisema hawapo tayari kuondoka katika makazi hayo na serikali kama ina nia ya kuwasaidia kuzifanyia matengenezo na sio kujengwa majengo mapya.

“Nyumba hizi historia yake kubwa tulivunjiwa nyumba na tukapewa fidia za nyumba nashangaa leo tunaambiwa nyumba zinavunjwa alafu tuhamishiwe ng’ambo ya mji,” alisema Abdallah Ali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live