Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtoto mchanga atupwa mlangoni Katavi

Mtoto Kichanga.jpeg Mtoto mchanga atupwa mlangoni Katavi

Mon, 3 Apr 2023 Chanzo: mwanachidigital

Mtoto mchanga anayekadiriwa kuwa na umri wa siku 14 amekutwa ametupwa kwenye mlango wa nyumba ya Jenifa Donald mkazi wa Tabukareli mtaa wa Shauritanga Manispaa ya Mpanda.

Wakizungumza na mwananchi Mashuhuda wa tukio hilo Paulo Daniel amesema akiwa anatoka matembezini saa 3:00 usiku Aprili 2, 2023 baada ya kuingia getini, alikuta kuna nguo kwenye mlango wa kuingia ndani kuna kitu kinachezacheza.

“Sikujua kama kuna mtoto sikugusa nikaingia ndani nikauliza mlangoni kuna nini, watu waliokuwa ndani wakatoka wakafunua tukakuta mtoto ameviringishwa kwenye nguo hii,”

“Tukachukua hatua ya kwenda kwa Mwenyekiti kufika pale hakuwepo tukampigia simu Mjumbe akaja haraka naye akampigia Mwenyekiti akaja wakashuhudia tunasubiri kwenda polisi,” amesema Paulo.

Wakazi wa eneo hilo wamesikitishwa na kitendo hicho Anna Willson amesema watu wengi wanalilia watoto wanakosa suala la kuchukua mtoto na kumtupa linaumiza.

“Nawaomba akina mama vitendo hivi waviache kama hawataki kubeba ujauzito watumie kinga zipo nyingi hospitalini kutupa mtoto ni kitendo cha kinyama sana,”

Naye Esta John amesema kinachosababisha wanawake kutupa watoto ni umasikini na wanaume wengi wanawarubuni wanawake kufanya nao mapenzi pasipo kuwaoa.

”Wanataka kudanga (kuzurura) tu hawaoi ndo inasababisha kutupwa watoto hivi, rai yangu kwa Serikali rais mama yetu aangalie janga hili wanaohusika wakamatwe wafungwe jela,”

Geofrey Kapola mkazi wa Tambukareli amesema licha ya wanawake wengi wanatoa kisingizio cha ugumu wa maisha kusababisha kutupa watoto sio kweli.

“Hakuna mtu anayeweza kushinikizwa kufanya tukio la namna hii bali ni akili zao wao wenyewe kwa sababu huyu mtoto hali chakula ananyonya maziwa ya mama pekee,”

“Ni akili zao tu waachane na habari za kubeba mimba, kweli wapo wanaume wanadanganya lakini hawezi kukudanganya mimba imefika hadi miezi 9 unadanganywa kabla ya kupata ujauzito,”amesema Kapola.

Mwenyekiti wa Mtaa huo Selestine Shauritanga amekiri kupokea taarifa za tukio hilo saa 3:45 usiku baada ya kupigiwa simu na Mjumbe wake.

“Nilikuja tukashuhudia nikahoji haukukutana na mtu getini alikataa, ni tukio la kwanza kutokea eneo hili lakini aliyefanya hivi siyo mkazi wa hapa wenye mimba nawafahamu wote,”

“Ni hawa wadangaji (wazururaji) amelewa pombe huko amepata danga (mwanaume) akaona atupe mtoto, rai yangu kwa wananchi wakimpata mhusika watoe taarifa akamatwe hivi sasa tunakwenda polisi,”

Mwananchi inaendelea kufanya jitihada za kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi ili kuzungumzia tukio hilo.

Chanzo: mwanachidigital