Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtoto anayeteseka kwa saratani aanza kusaidiwa

Mtoto anayeteseka kwa saratani aanza kusaidiwa

Wed, 19 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam.  Mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania, Mohammed Dewji ‘Mo’ na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ni miongoni mwa watu waliojitokeza kumsaidia mtoto wa miaka mitatu, Said Alli mkazi wa  Zanzibar anayeteseka na maradhi ya saratani.

Tangu jana Jumanne Februari 18, 2020 video na picha za mtoto huyo akiwa katika hali mbaya zilianza kusambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii huku ndugu na jamaa wakiomba msaada aweze kupata matibabu.

Picha hizo zinamuonyesha mtoto huyo akiwa amebabuka sehemu kubwa ya mwili wake hasa usoni, ana vipele vidogo. Mtoto huyu muda mwingi analia jambo linaloashiria kuwa ana maumivu makali. Wengi wanaofika kumjulia hali huishia kutokwa machozi.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Februari 19, 2020, Rashid Salum anayemsaidia mtoto huyo amesema hatua za awali za matibabu zimeanza baada ya Serikali ya Zanzibar kumsaidia.

Amesema mtoto huyo anasumbuliwa na saratani ya ngozi na baada ya vipimo watajua kama wanaweza kumsafirisha kwenda jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu zaidi.

“Tunashukuru Serikali ya Zanzibar imeanza kumsaidia mtoto na hatua za awali za vipimo zimeanza. Tukipata majibu tunaweza kuja Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu zaidi,” amesema Rashid.

Pia Soma

Advertisement
Katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Makonda ameandika, “nakosa amani naomba nimpeleke hospitali huyu mtoto, tangu jana usiku sijalala nilipoona clip yake najua maumivu ya wazazi ni zaidi ya mtoto mwenyewe.”

Naye Mo amesema, “nimeguswa sana na hali ya mtoto wetu, kupitia taasisi yetu ya Mo Dewji Foundation tutagharamia matibabu yake yote kupita Hospitali ya Muhimbili wodi ya saratani kwa watoto. Tunaomba mawasiliano ya mzazi, nipo tayari kusaidia Insha’llah.”

Waziri wa Afya Zanzibar, Hamad Rashid akiwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja mjini Unguja wodi ya wagonjwa wa ngozi amesema Serikali haijashindwa kuwahudumia wananchi wake hivyo sio vyema kusambaza picha ya mgonjwa katika mitandao ya kijamii.

“Kusambaza picha ya mgonjwa katika mitandao ya kijamii ni kosa la kumdhalilisha,” amesema Hamad.

Chanzo: mwananchi.co.tz