Dar es Salaam. Editha Kakula (11), anayeishi Makongo jijini Dar es Salaam aliyepotea tangu Januari 9, 2019 amepatikana leo jioni Januari 15, 2019.
Mtoto huyo mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi City iliyopo Makongo Juu, aliondoka nyumbani baada ya kutoka shule, kupanda daladala na jirani yake ambaye amesimulia jinsi walivyoachana kituoni, huku mtoto huyo akisema anakwenda kwa shangazi yake.
Kamanda wa Polisi mkoa wa kipolisi Kinondoni, Jumanne Muliro amesema hadi leo saa 10 jioni, polisi walikuwa wakiendelea na uchunguzi.
Mlezi wa mtoto huyo, Burchard Kakula akizungumza na Mwananchi leo amesema amepatikana katika maghorofa ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yaliyopo Makongo karibu na nyumbani kwao.
Amesema Editha alikwenda katika nyumba hizo kumuulizia rafiki yake ambaye alimtambulisha kwa wazazi wake ambao walimpigia simu.
Kakula amesema baada ya kufika katika nyumba hiyo hakuamini alipomuona Editha akiwa salama, kumchukua hadi kanisani kwa ajili ya maombi.
Alivyopotea
Jirani wa mtoto Editha aliyeomba jina lake kuhifadhiwa, aliliambia Mwananchi kuwa Januari 9, alimuona Editha katika kituo cha daladala Makongo akamuuliza anakoelekea na kujibiwa na mtoto huyo kuwa ametumwa na mama yake kwenda Tegeta.
“Tulipanda wote gari na tukateremka pamoja pale Tegeta kwa Ndevu. Nikataka kumvusha barabara ila alikataa, kuniambia kuwa anakwenda kwa shangazi yake, alivuka barabara na kwenda zake,” amesema mama huyo.
Hawa Yahaya ambaye ni mtoto wa mama huyo, anayesoma na Editha darasa moja, amesema siku ambayo rafiki yake amepotea alimueleza kuwa hataki kurejea nyumbani kwa sababu alikuwa amefanya kosa.
“Nilimuuliza sasa kama huna hamu ya kurudi nyumbani utakwenda wapi, lakini alininyamazia kimya. Baada ya masomo tulicheza na ulipofika muda wa kutoka shule tulipanda gari tulimshusha getini na akaongozana na mtoto anaitwa Patrick kwenda nyumbani kwao,” amesema Hawa.
Awali akizungumzia tukio hilo, Kakula amesema Januari 9, gari la shule lilimfuata Editha asubuhi na kumrudisha jioni, kwamba waliporejea nyumbani walikuta nguo zake za shule lakini yeye hakuwepo.
Amesema mtoto huyo hakurejea nyumbani siku hiyo na hata alipomuuliza mama yake kama amemtuma, alieleza kuwa hakumtuma sehemu yoyote.
“Tulimtafuta kwa ndugu na jamaa wa karibu bila mafanikio na kwa marafiki zake ambao walisema hawajamuona. Tuliamua kuripoti kituo cha polisi cha Kawe na kupewa RB namba KW/RB/297/2019,” amesema Kakula.