Mtoto Jafari Bakari mwenye umri wa miaka 16, mkazi wa Kijiji cha Mnima, Kata ya Mnima mkoani Mtwara, anadaiwa kujinyonga porini kisa Sh. 8,000 aliyokuwa akidaiwa na rafiki yake.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Kamishna Msaidizi wa Polisi Isack Mushi alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea majira ya jioni baada ya Jafari kuondoka nyumbani kwao na kwenda kusikojulikana.
Alisema kwa mujibu wa mashuhuda walioona mwili huo, waliukuta porini ukiwa unaning'inia juu ya mti kwa kutumia kamba ngumu.
Kamanda alisema chanzo cha kifo hicho kimetokana na mwili kukosa hewa ya kutosha baada ya kubanwa na kamba aliyoitumia kujinyonga.
Alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtoto huyo alikuwa anadaiwa Sh. 8,000 na rafiki yake ambapo hata hivyo mama wa marehemu alizilipa ili kuondoa usumbufu kati yao.
Alisema kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kubaini sababu za kufanya uamuzi wa kujinyonga.
Dada wa marehemu, Sharifa Bakari alisema kuwa kabla ya mwili huo kukutwa porini, alimwona akipigwa vibaya na kijana ambaye hakumfahamu, hali iliyomsababishia kuingiwa na wasiwasi.
Alisema kuwa baada ya kipigo hicho alimwona mdogo wake akikimbilia maeneo ya porini na alipomfuatilia alikuta akiwa amejinyonga kwa kamba.
"Imeniumiza sana kifo cha mdogo wangu kwa sababu nimeshuhudia kwa macho yangu kabla ya kujinyonga, amepigwa kipigo kibaya, na nikamwona anakwenda porini nilipofuatilia kumbe alipigwa kwa ajili ya deni la Sh. 8,000 na ndipo kaamua kujinyonga," Sharifa alidai.
Selemani Mtunga, mkazi wa kijiji hicho alidai kuwa majira ya saa 12 jioni alimwona mtoto huyo anapigwa maeneo mbalimbali ya mwili na kijana aliyemtaja kwa jina moja la Mkuruduku.
"Alieleza kuwa anamdai (Jafari) Sh. 8,000 na kwamba alipokwenda kununua samaki na alitoa Sh. 2,000 na kutaka samaki ila kwa bahati mbaya, alirudishiwa Sh. 10,000 na hakurudisha hata baada ya kufuatwa," alidai.