Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mti ulionyongea watu Mwanza waondolewa

48894 Pic+mti

Wed, 27 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Mti maarufu wa mkuyu uliokuwa katika mzunguko wa barabara ya Nyerere, Kenyatta na Makongoro karibu na ofisi za CCM Mkoa wa Mwanza umeondolewa na sasa limewekwa shina lenye mfano wa mti huo.

Awali, katika eneo hilo kulikuwa na mti uliotumiwa na wakoloni kuwanyongea Waafrika enzi za utawala wao.

Kabla ya ukoloni, mti huo kwa mujibu wa wazee wa jiji hilo ulitumika kwa shughuli za matambiko ya wenyeji.

Baada ya ukoloni kuingia nchini, ulibadilika kutoka eneo la tambiko hadi kuwa sehemu ya kuwanyongea wakosaji waliotiwa hatiani wakati wa utawala wa Wajerumani.

Janepaa Trome (94), mkazi wa jijini Mwanza, anasema mti huo ulikuwa mkubwa kuliko miti yote eneo hilo na vilevile ulikuwa umepakana na eneo maalumu lililokuwa linatumika kama jela.

Anaeleza kuwa watu walinyongwa asubuhi na kubaki kwenye kamba hadi jioni kisha kukabidhiwa familia zao kwa ajili ya mazishi. “Unaona pale Moili, ndipo kulikuwa na jengo la kuwahifadhi watu waliohukumiwa kifo na kutoka pale hadi hapa haikuwa mbali. Kila mtu aliyestahili adhabu ya kifo alinyongwa siku yake maalumu,” anasema.

Raphael Muruga (67) anasema kwa mujibu wa maelezo kutoka kwa wazee, mjomba wake, Benedicto Merengo ndiye alikuwa mlinzi wa mti huo wa kunyongea Waafrika waliokuwa si watiifu kwa wakoloni.

Uhifadhi wa eneo

Baada ya Uhuru wa Tanganyika Desemba 9, 1961 mti huo ulisalia eneo hilo kama kumbukumbu ambayo hata hivyo haikujulikana kwa wengi.

Ofisa uhusiano wa Jiji la Mwanza, Elirehema Kaaya anasema halmashauri ilifikia uamuzi wa kukata matawi yake kabla, na baadaye kulazimika kuukata na kusalia shina kutokana na ukubwa wake.

Anasema baadaye uongozi uliamua kujenga sanamu maalumu ya shina linalofanana na lile wa awali ili kudumisha historia ya eneo hilo.

Anasema ujenzi wa sanamu hiyo ulioanza Desemba 10, 2018 umekamilika Januari 28 na kugharimu zaidi ya Sh13.6 milioni zilizotolewa na jiji rafiki la Wurzburg, Ujerumani.

“Siku zote huwezi kuifuta historia, iwe mbaya au nzuri daima itabaki kuwa tu historia; ndiyo maana licha ya historia ya mti ule kuwa na kumbukumbu inayoumiza miongoni mwa Watanzania, bado jiji limeona ni busara kuudumisha kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema Kaaya.

“Sanamu hii itakuwa moja ya vivutio vya utalii jijini Mwanza na halmashauri itafunga taa maalumu ya umeme jua kuwezesha wageni kuuona mti huo kwa saa 24.”

Kwa mujibu wa Sera ya Malikale ya 2008, mti huo ni malikale inayopaswa kutunzwa kutokana na kuwa na sifa za rasilimali za urithi wa utamaduni zenye umri wa miaka 100 na kuendelea.



Chanzo: mwananchi.co.tz