Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtendaji Mkuu amuagiza mkandarasi kumaliza haraka ukarabati MV Tanga

PIC 2 768x432 Mtendaji Mkuu amuagiza mkandarasi kumaliza haraka ukarabati MV Tanga

Tue, 8 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Lazaro N. Kilahala, Tarehe 7 Novemba 2022, amekagua ukarabati unaoendelea wa kivuko cha MV.TANGA kinachofanyiwa ukarabati mkubwa katika eneo la Pangani Mkoani Tanga na kumuagiza mkandarasi kuhakikisha anamaliza ukarabati huo haraka iwezekanavyo ili kivuko hicho kirejee kutoa huduma katika eneo hilo.

Kilahala amekagua ukarabati wa kivuko hicho akiambatana na Meneja wa TEMESA Tanga Mhandisi Jairos Nkoroka Pamoja na Mkurugenzi wa Huduma Saidizi Bi. Josephine Matiro, Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi Mhandisi Hassan Karonda na Mkuu wa Kivuko cha Pangani Bweni Mhandisi Abdulrahman Ameir.

Mkandarasi, Kampuni ya Dar es Salaam Maritime Group inayosimamia ukarabati wa kivuko hicho Mhandisi Michael Wlson aliahidi kumaliza ukarabati huo ndani ya mwezi huu wa Novemba.

Awali Mtendaji Mkuu alitembelea karakana ya Mkoa wa Tanga na kuzungumza na watumishi ambapo aliwaagiza kubadili namna wanavyofikiri kwani miongoni mwa mabadiliko makubwa kabisa yanayotakiwa kutokea TEMESA, badiliko kubwa ni namna ya kufikiri kibiashara zaidi.

Kilahala amesema sehemu kubwa ya tatizo la TEMESA ilikuwa ni kutokutambua kwamba kuna tatizo hivyo akaupongeza uongozi wa Mkoa huo chini ya Meneja wa Mkoa Mhandisi Jairos Nkoroka kwa kutambua kwamba kuna tatizo na kuonyesha ari ya kutatua matatizo yaliyopo huku akiwasisitizia kubadili mitazamo ya utendaji kazi na kutatua yale ambayo yamekuwa yakilalamikiwa siku zote.

"Niwape changamoto menejimenti yenu, mjielekeze katika namna gani kituo chenu kitaweza kujiendesha na kuwa kituo cha biashara ambacho kipo kibiashara zaidi na kinatengeneza mapato yake ya kukiwezesha kujitegemea,” Alisema Kilahala.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live