Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtatiro awakaribisha watoro 12 ikulu ndogo

82912 Pic+mtatiro Mtatiro awakaribisha watoro 12 ikulu ndogo

Wed, 6 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro amewakaribisha nyumbani kwake (ikulu ndogo) wanafunzi 12 wanaotuhumiwa kwa utoro sugu.

Mkuu huyo wa wilaya alisema atakaa na wanafunzi hao wa shule mbalimbali za Tunduru kwa siku tatu za mwisho wa wiki yaani Ijumaa, Jumamosi na Jumapili.

Alisema atawaalika wanafunzi hao Ijumaa wiki hii na atakaa nao mpaka Jumatatu watakapokwenda shule.

“Watoto hao wote ni wa kiume, kati ya hao 12, watatu ni wa shule ya Ligoma. Wana matatizo makubwa, nataka kuwa nao ili niwasaidie kisaikolojia,” alisema.

Baadhi ya wanafunzi hao ni wale walioadhibiwa wiki iliyopita kwa kosa hilo la utoro sugu.

Mtatiro alisimamia adhabu ya watoro wa Shule ya Sekondari Ligoma wilayani humo, ambao walichapwa viboko mbele ya wenzao na wazazi wao, Alhamisi iliyopita. Ilikuja siku chache baada ya mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila kuwachapa viboko wanafunzi 14 wa Shule ya Sekondari Kiwanja kwa tuhuma za kuchoma moto mabweni ya shule hiyo na kukutwa na simu, Oktoba 3, mwaka huu.

Hata hivyo, Mtatiro alimuagiza mwalimu wa shule ya Ligoma iliyopo Tarafa ya Namasakata awachape viboko vinne wanafunzi hao na pia kutaka wapewe adhabu nyingine ya kuchimba visiki.

Akizungumza katika mahojiano maalumu alipotembelea ofisi za kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) inayochapisha gazeti la Mwananchi, mwishoni mwa wiki, Mtatiro alisema lengo la kuwakaribisha wanafunzi hao ni kuwapa msaada wa kisaikolojia ili waanze maisha mapya.

“Mimi ni `mentor’ (mshauri) mzuri, nikimaliza kazi zangu za ofisini mara nyingi naenda katika shule kuzungumza na wanafunzi na walimu na pia ujue kazi hii nimeifanya kwa miaka mingi.

“Wakija nyumbani nitakaa nao kama familia, nitazungumza nao, kula chakula na kuangalia mpira huku nikiwashauri masuala mbalimbali ya maisha yao, kubwa zaidi ni umuhimu wa elimu,” alisema Mtatiro.

Mkuu huyo wa wilaya alisema wanafunzi hao wamepatikana baada ya kuendesha operesheni maalumu ya kuwabaini wanafunzi watoro baada ya kuwakamata na kuwaweka ndani wazazi wao.

Alisema kilichomsukuma kuchukua hatua hiyo ni mwenendo mbaya wa mahudhurio ya wanafunzi katika wilaya hiyo ambako katika shule za sekondari hali ni mbaya zaidi.

“Nilianza operesheni hii Oktoba 18, mwaka huu na itaendelea mpaka mwaka 2020 na hadi sasa tumebaini watoro 60. Sasa hao 12 ndio nitawakaribisha nyumbani,” alisema Mtatiro.

Mtatiro alisema katika siku ya kwanza alipoanza kampeni hiyo watoro watatu walikamatwa pamoja na wazazi hao na akaamuru wakae ndani kwa saa tano kabla ya kupelekwa shuleni na kupewa adhabu ya viboko.

“Lengo la kampeni hii ni kuwajengea mazingira watoto na wazazi wao kujua wajibu wao katika elimu,” alisema Mtatiro.

Mtatiro alisema amegundua wanafunzi hao wanaacha shule kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo umbali mrefu, kutokutambua thamani ya elimu na mambo ya unyago.

“Hali ni mbaya sana, watoto wanaanza kufundishwa masuala ya unyango na jinsi ya kumhudumia mwanaume wakiwa na umri mdogo sana kuanzia miaka mitano tu, jambo linalosababisha kutamani kwenda kufanya kwa vitendo,” alisema Mtatiro.

Alisema kutokana na sababu hizo ameona ni bora kuwasaidia kisaikolojia watoto hao kwa kuzungumza nao na kuwapa mifano ya watu waliofanikiwa kutokana na elimu licha ya changamoto walizopitia.

Alisema kwa sasa kipaumbele chake kikuu ni elimu na atahakikisha hilo linatekelezeka ili siku moja atakapoondoka aache urithi bora kwa wananchi wa wilaya hiyo.

“Takwimu za sasa za elimu katika wilaya yangu siyo nzuri, kwa upande wa shule ya msingi angalau tunafanya vizuri na mwaka huu, moja ya shule zetu imeshika nafasi ya tatu kitaifa katika mtihani wa kuhitimu darasa la saba, hali ni mbaya kwa sekondari,” alisema.

Mtatiro alisema kati ya wanafunzi 150 wanaojiunga na sekondari, theluthi moja sawa na wanafunzi 40 mpaka 50 hawamalizi shule kutokana na tabia ya utoro sugu.

Alisema hali hiyo ni hatari sana kwa maendeleo ya wilaya hiyo kwani inakosa watu walioenda shule na matokeo yake watoto wengi kukimbilia katika miji mikubwa ikiwamo jijini Dar es Salaam na kujihusisha na kazi za ndani, ombaomba, uhudumu wa baa na biashara haramu za kuuza miili yao.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni mimba; “Hili tatizo ni kubwa kwetu na tumebaini watoto kadhaa baada ya kuletwa na wazazi wao.

“Hapa `interest’ (nia) ni kujua aliyempa mimba mwanafunzi, mjawazito anahojiwa na polisi amtaje na tayari tumeshawakamata watu kadhaa na wako chini ya ulinzi wakisubiri taratibu za mahakama.”

Chanzo: mwananchi.co.tz