Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema itamchukulia hatua Moses Mollel maarufu Nabii Namba Saba iwapo atashindwa kudhibitisha kauli yake kuwa ana uwezo wa kutibu wenye maambukizi ya virusi vya corona.
Hayo yameelezwa na naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile katika ziara yake ya kikazi jijini Arusha.
Nabii Namba Saba, mkazi wa Ngaramtoni wilayani Arumeru mkoani Arusha amekuwa akijitangaza kuwa na dawa ya kutibu ugonjwa huo na kuweka mawasiliano yake kwenye mitandao.
Dk Ndugulile amesema taarifa za mtu huyo zimesambaa katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, kumtaka athibitishe.
Amesema Serikali imetuma wataalamu wake kumsaka na kumhoji kama anavyo vibali vya kutoa huduma ya tiba na kujitangaza.
“Kimsingi nimeiona hiyo taarifa ya huyo mtu anayejiita Nabii Namba Saba kuwa ana dawa ya kutibu ugonjwa wa Corona, ila hapa Tanzania hatuna maambukizi yoyote ya ugonjwa huo tunachotaka huyo mtu atuthibitishie uwezo wake wa kutibu huo ugonjwa wa corona,” amesema Dk Ndugulile.
Habari zinazohusiana na hii
- Wagonjwa 4,740 wapona virusi vya corona
- Waliokufa kwa corona wazidi 900
- Virusi vya corona, vyaua 242 kwa siku moja
- VIDEO: WHO yapata jina rasmi la ugonjwa wa corona
Dk Ndugulile amesema yeyote anayetoa tiba asili na mbadala lazima asajiliwe na Wizara ya Afya, dawa zake ziwe zimesajiliwa na Wizara hiyo na kusisitiza kuwa nabii huyo pia anapaswa kuthibitisha amesajiliwa wapi na lini.