Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtanzania aliyejinyonga Kenya azikwa kwao Gonja

3b0a61647cda5dff96a086e1816375c7 Mtanzania aliyejinyonga Kenya azikwa kwao Gonja

Fri, 11 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KIJANA Rashidi Mberesero aliyejinyonga katika Gereza la Kamiti nchini Kenya, amezikwa jana huko Gonja wilayani Same mkoani Kilimanjaro.

Mberesero alikuwa akitumikia kifungo cha maisha katika gereza hilo, baada ya kukutwa na hatia katika kesi iliyokuwa ikimkabili.

Familia ya marehemu imeishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutokana na msaada mkubwa waliotoa na kufanikisha kupata mwili wa kijana wao.

Baba mzazi wa marehemu, Charles Mberesero alisema hayo jana alipozungumza na HabariLEO ambapo aliishukuru pia serikali ya Kenya kwa kukubali kuwapa mwili wa kijana wao, ambaye alihukumiwa kwenda jela maisha baada ya kukutwa na hatia ya kuhusika katika mashambulizi ya kigaidi katika Chuo Kikuu cha Garissa nchini Kenya.

“Pia tunaushukuru ubalozi wetu wa Kenya kupitia Balozi George Simbachawene na msaidizi wake, Talha Mohammed kwa mchango wao mkubwa ambao uliotusaidia kuupata mwili wa kijana wetu,” alisema Mberesero.

Alisema familia yake iliwasili jijini Nairobi siku ya Jumatatu na kufanikiwa kupata mwili wa kijana wao siku ya Jumatano na kumhifadhi katika makazi yake ya milele jana huko Gonja wilayani Same mkoani Kilimanjaro.

“Tulipata ushirikiano wa hali ya juu kutoka katika Jeshi la Magereza nchini Kenya kutoka ubalozi wetu Kenya kwa kweli tunawashukuru sana kwa kuwa tayari tumeupata mwili wa kijana wetu na tunamzika leo (jana) hapa Gonja,” aliongeza Mberesero.

Rashidi Mberesero alihukumiwa na wenzake wawili, Hassan Edin na Mohamed Abdi, raia wa Kenya, waliofungwa kifungo cha miaka 41 kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika katika shambulio la kigaidi katika Chuo Kikuu cha Garisa Aprili mwaka 2015, ambapo watu zaidi ya 150 walipoteza maisha.

Vijana hao watatu walitiwa hatiani, kwa kula njama na kufanya shambulio la kigaidi kwa kushirikiana na kundi la kigaidi la Al-Shabaab lenye maskani yake katika nchi jirani ya Somalia.

Kundi hilo limehusika katika matukio kadhaa nchini Kenya, likiwemo la West Gate ambapo magaidi ya Al-shabaab waliwaua wananchi wa Kenya zaidi ya 60 na kujeruhi mamia wengine.

Chanzo: habarileo.co.tz