Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtanzania aliyefia Israel kuzikwa leo

Mtanzania Clemence Kuzikwa.png Mtanzania aliyefia Israel kuzikwa leo

Tue, 28 Nov 2023 Chanzo: mwanachidigital

Mwili wa Clemence Mtenga (22), Mtanzania aliyeuawa vitani nchini Israel, umewasili nyumbani kwao katika Kijiji cha Kirwa, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro na kuibua vilio na simanzi kutoka kwa ndugu na mamia ya waombolezaji waliofika nyumbani hapo.

Mwili huo umefikishwa nyumbani kwa ajili ya ibada fupi ya kumuombea marehemu Mtega na baadaye utapelekwa kanisani, katika Parokia ya Mashati kwa ajili ya ibada takatifu ya maziko, kisha kurudishwa nyumbani kuhitimisha safari yake duniani.

Msafara wa kuutoa mwili huo katika Hospitali ya Huruma ulikokuwa umehifadhiwa, uliongozwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Rombo na ulipofika nyumbani, jeneza limebebwa na askari wa Jeshi la Akiba (mgambo).

Kutokana na mazingira ya mwili huo, imeelezwa kuwa hautaonyeshwa hadharani, isipokuwa waombolezaji watauaga kwa kuangalia picha yake itakayowekwa juu ya jeneza.

Mwili wa Mtega uliwasili nchini jana Novemba 27, 2023, saa 2:51 usiku, kwa ndege ya shirika la Uholanzi (KLM), kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ambapo ulipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu.

Novemba 17, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ilithibitisha kupokea taarifa za kifo cha Clemence Mtenga, ambaye alikuwa miongoni mwa Watanzania wawili ambao pamoja na raia wa mataifa mengine, walikuwa hawajulikani walipo baada ya kuanza kwa vita kati ya Hamas na Israel.

Clemence alikuwa miongoni mwa vijana wa Kitanzania 260 waliokwenda Israel kushiriki mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa vitendo, chini ya mpango wa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Israel.

Chanzo: mwanachidigital