Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Jumanne Sagini amesema wanawake na mabinti 16 wanaojihusisha na mtandao wa matendo maovu ikiwemo mitandao ya ngono wamekamatwa Jijini Dar es salaam na taratibu za kuwafikisha mahakamani zinaendelea.
Wanawake hao wamekamatwa katika maeneo mbalimbali Jijini Dar es salaam yakiwemo Mwananyamala, Kinondoni, Mkwajuni, Tandale, Sinza na Buza.
Akizungumza na wanahabari Naibu Waziri Sagini akiwa na Kamanda wa Polisi Kanda maalumu Dar es salaam Muliro Jumanne Muliro amesema kumekuwa na ongezeko la makundi ya wanawake wanaofanya matendo yanayokiuka maadili na kuyatangaza katika mitandao ya kijamii.
Baadhi ya matendo hayo ameyataja kuwa ni kucheza ngoma zijulikanazo kama kibao kata na vigoma hasa nyakati za usiku huku wakiwa wamevaa mavasi yasiyo na maadili
Mengine ni kuibuka kwa wanawake wanaofundishana kufanya matendo ya ngono kwa kutumia vifaa hatarishi kama chupa za bia, soda, mahindi ya kuchoma, ndizi na matango huku baadhi wakiunda makundi kwenye mitandao ya kijamii na kuweka picha zao.
Naibu Waziri amesema baadhi ya wanawake wanaoshiriki matendo hayo husafirishwa kwenda ughaibuni na kutumikishwa katika biashara ya ukahaba jambo ambalo ni kinyume na sheria za nchi.
Amesema kufuatia agizo la Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alilotoa hivi karibuni kuhusu kuporomoka kwa maadili na kuagiza viongozi kushughulika nalo tayari vyombo vya dola vimeanza kazi ya kukomesha matendo hayo.