Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtaka: Mwanafunzi mtukutu afukuzwe shule, asichapwe

Antony Mtaka Mkuu Wa Mkoa Wa Njombe.png Mtaka: Mwanafunzi mtukutu afukuzwe shule, asichapwe

Mon, 20 Mar 2023 Chanzo: mwanachidigital

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amewaagiza wakuu wa shule za Serikali kuwafukuza wanafunzi watukutu badala ya kuwachapa viboko au kuwarudisha nyumbani.

Mtaka alisema hayo alipozungumza na wanafunzi wa Sekondari ya Wasichana ya Manyunyu, iliyopo Matembwe wilayani Njombe.

Alisema shule si sehemu za watu kufanya mizaha na wazazi wengi wanaheshimu sana shule binafsi lakini za Serikali mambo huwa tofauti.

Alisema zipo shule za watu binafsi zikitoa maelekezo wazazi wengi wanayafuata, lakini kwa shule za Serikali wanaleta mzaha.

“Kuna shule za binafsi zikiagiza mwanafunzi aje na nguo mbili wanaenda nazo hizohizo, ukienda na ya tatu unarudishwa, wanakuambia shule hii ni marufuku mtoto kuja na simu ukienda nayo unarudishwa nyumbani, huku kwenye shule zetu za umma tuna mizaha mingi,” alisema.

Mizaha hiyo alisema inasababisha mwanafunzi akifanya vituko na mwalimu akamwadhibu basi mwalimu atajadiliwa hadi kwenye mitandao ya kijamii na polisi watamkamata kuandika maelezo, lakini ujinga huo haufanyiki shule binafsi.

Alisema jamii inapozungumzia maadili ni lazima yasimamiwe na namna ya kuyasimamia ni kuyajenga tangu vijana wakiwa shuleni.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Valentino Hongoli alisema “mwaka jana mheshimiwa Rais alitupatia Sh60 milioni ambazo tulijenga madarasa matatu na ofisi shuleni hapa, kama tusingepewa watoto wangeshindwa kusoma.”

Mkuu wa Sekondari ya Wasichana Manyunyu, Advera Bagoka alisema wanafunzi waliotakiwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu walikuwa 202, ila walioripoti ni 120 na 51 wamebadilisha shule, huku 31 hawajulikani walipo.

“Shule yetu ina uhaba wa walimu wa sayansi na hisabati,” alisema.

Chanzo: mwanachidigital