Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msimamizi wa mali za bilionea Olomi kujulikana Mei 28

Wed, 22 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Mahakama Kuu Moshi inatarajia kutoa hukumu ya usimamizi wa mirathi ya  bilionea  Jubilate Olomi  aliyefariki  Januari 15, mwaka huu Jijini Nairobi Kenya, Mei 28, mwaka huu.

Bilionea Ulomi, amefariki na kuacha magari kadhaa ya kifahari, nyumba katika miji ya Mererani, Arusha, Moshi, migodi ya Tanzanite, mashamba na mali nyingine kadhaa, maeneo mbalimbali nchini zenye thamani ya mabilioni ya fedha.

Mdogo wa marehemu, Werandumi Olomi aliomba Mahakama Kuu kumuidhinisha kusimamia mirathi hiyo, lakini amepingwa na mke wa marehemu, Zainabu Rashid na mtoto wake, Julius Julibate.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Dk Fauz Twaib  ambaye  ndiye anasikiliza kesi hiyo, alitarajia leo kutoa uamuzi lakini ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 28, atakaposoma hukumu.

Katika kesi hiyo, Wakili wa Werandumi Ulomi anatetewa na Wakili Joseph Ngiloi  wakati mjane wa marehemu na mtoto, wanatetewa na wakili Engelberth Boniphace.

Awali,  Wakili Ngiloi alimwekea pingamizi wakili Boniphace  kuendelea kumtetea mjane huyo na mtoto wa marehemu kwa madai kuwa ni mtumishi wa halmashauri, hana leseni ya biashara na anavunja sheria za utumishi wa umma.

Pia Soma

Hata hivyo, Jaji Twaib alitupilia mbali pingamizi hilo  na kueleza kuwa wakili huyo anatambuliwa kisheria kama wakili na amefuata utaratibu wote wa kuwa wakili ikiwapo kumiliki leseni ya uwakili.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi jana,  Wakili Ngiloi alisema  tayari ameandika notisi ya kukata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga maamuzi ya Mahakama Kuu kanda ya Moshi.

“Tayari nimeandika notisi ya kukata rufaa na tutaiwasilisha mahakamani, bado tunaamini Wakili Boniphace hapaswi kuendelea kuwa wakili katika shauri hili,” amesema.

Awali, kabla ya mgogoro huo wa kugombea usimamizi wa mirathi kufikishwa mahakamani, uliibuka mgogoro wa kugombea mwili na kutaka kuzika ambao ulifikishwa kwa  Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na baada ya kushindwa kuelewana pande zote, alishauri mgogoro huo kufikishwa mahakamani hata hivyo, ndugu wa Olomi walipata haki ya kuzika.

Chanzo: mwananchi.co.tz