Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msamalia aliyemwokota mtoto na kumlea, anyang'anywa

Mtoto Kichanga.jpeg Msamalia aliyemwokota mtoto na kumlea, anyang'anywa

Fri, 3 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Madwiani wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara wamemtaka Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Masumbuko Mtesigwa, kumrejesha Masasi mtoto aliyeokotwa jalalani kisha kuchukuliwa na kupelekwa mkoani Tanga katika mazingira yenye utata.

Viongozi hao wamedai kuwa mtoto huyo aliokotwa jalalani Masasi mwaka jana akiwa na umri wa siku mbili na kulelewa na mkazi wa Kijiji cha Chiunguta, Ziada Daniel na juzi alichukuliwa na moja ya familia kutoka Tanga wakidai ni mtoto wao.

Pia walieleza kuwa familia hiyo walisafiri kutoka Tanga hadi wilayani Masasi kwa ajili ya kumchukua mtoto huyo kwenda kumlea mkoani Tanga.

Walitoa maagizo hayo wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani, wakisema kitendo kilichofanyika cha kumnyang’nya mtoto mama huyo ambaye tangu ameokotwa aliamua kujitolea kumlea hadi anafikisha umri wa mwaka mmoja, hakikubaliki.

Diwani wa Mwena, Nestory Chilumba alisema mama huyo ameonyesha moyo wa mapenzi na mtoto huyo tangu akiwa mchanga.

Alisema wanashangazwa kusikia kuna mama na mume wake wametoka mkoani Tanga hadi Masasi na kumchukua mtoto huyo kinyemela.

Alisema Ziada ametumia gharama kubwa kumlea mtoto huyo ambaye alikabidhiwa na Serikali ya Wilaya ya Masasi kumlea.

"Tunakuagiza mkurugenzi haraka ufanye jitihada za kuhakikisha mtoto huyu anarudi Masasi na anakabidhiwa mama huyu aendelee kumlea. Haiwezikani mtoto ameokotwa Masasi na alishajitokeza wa kumlea halafu anyang’anywe na kupewa mtu kutoka Tanga, tunaka mtoto arudi Masasi haraka," alisema Chilumba.

Diwani wa Viti Maalum, Asina Lipopola alisema: "Sisi madiwani wanawake tumeumia moyo kusikia mtoto huyo amesafirishwa kwenda mkoani Tanga huku mama ambaye awali alibeba majukumu ya kumlea kichanga akiwa bado na mapenzi na mtoto huyo."

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Ibrahimu Chiputula alisema baraza hilo halijaridhishwa na taarifa ya mtoto huyo kupelekwa Tanga na kunyng’anywa mama huyo.

Mama mlezi wa mtoto huyo, Ziada aliiambia Nipashe kuwa alikabidhiwa mtoto huyo kumlea na ustawi wa jamii mwaka jana, muda mfupi baada ya mtoto huyo kuokotwa jalalani.

Alisema anashangaa kuona wanakuja watu kutoka mkoani Tanga na kueleza wamekuja kumchukua mtoto huyo ili wakamlee.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Mtesigwa, alisema amepokea maagizo hayo ya madiwani na atayafikisha kwenye vyombo husika ili yafanyiwe kazi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live