Handeni. Katika kumaliza changamoto ya uhaba wa miundombinu shuleni, Wilaya ya Handeni imeanzisha mtindo wa 'Msalagambo' wa kuwajumuisha wazazi na walezi kushiriki kwenye shughuli za ujenzi wa madarasa.
Kupitia Msalagambo, kila Jumamosi wananchi hukutana kushiriki ujenzi wa madarasa kwenye shule za vijiji vyao ili kumaliza uhaba uliopo.
Akizungumza kwenye wiki ya elimu inayoendelea wilayani kwa ufadhili wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenmet) leo Jumatatu Mei 27,2019, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe amesema walikuwa wanakabiliwa na uhaba wa madarasa 62.
“Kupitia 'Msalagambo' ujenzi wa madarasa haya umefikia asilimia 90 kwa sababu wananchi wakijitolea, Serikali inaongezea nguvu, kwenye kila Msalagambo sisi viongozi hatukosekani,” amesema Gondwe.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella amesema mkakati uliopo mkoani humo ni kuhakikisha wanaongeza ufaulu na kuondoa sifuri.
Pia Soma
- MADAI: DPP awatuhumu wabunge kwa rushwa, Spika ajibu
- Utalii wa utamaduni washika kasi Japan
- Kesi washitakiwa wa meno ya tembo ya Sh1.466 bilioni Juni 11 na 12
- Watoto 20 kuzibuliwa mishipa na kuzibwa matundu ya moyo kwa Cath Lab
Amesema wamekamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara na kwamba katika bajeti ya mwaka 2018/2019 na 2019/2020 kipaumbele ni vifaa kwa ajili ya maabara hizo.
Awali, Mwakilishi wa Mratibu wa Tenmet, Clement Mganga amesema sababu ya kuchagua wilaya ya Handeni ni mfululizo mzuri wa matokeo mazuri ya darasa la saba na sekondari wanayoyapata mwaka hadi mwaka.
Ufaulu wa darasa la saba Handeni Vijijini umepanda kutoka asilimia 73.5 mwaka 2017 hadi 81.6 mwaka 2018 wakati Handeni mjini ni asilimia 78 hadi asilimia 80 mwaka jana.