Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel amesema zaidi ya bilioni 3 zilizokopwa katika halmashauri za Mkoa huo kupitia vikundi vya ujasiriamali hazijazirejeshwa kutokana na ukosefu wa elimu ya fedha.
Fedha hizo ni zile za asilimia 10 zinazokopeshwa na halmashauri kwa vikundi mbalimbali ikiwemo watu wenye ulemavu ,vijana na wanawake.
Amesema ukosefu wa elimu ya fedha kwenye jamii imepelekea kutokea kwa jambo hilo na kushauri vituo vya fedha kutoa mafunzo ya biashara na utunzaji fedha kabla na baada ya kukopa.
"Kuna fedha ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ambayo hutolewa kwa makundi maalum, ambayo ni vijana, wanawake, na wale wenye mahitaji maalum, ni vyema kujitathimini pia, je hawa watu wanapata elimu ya fedha? nidhamu ya fedha, tuangalie viashiria hatarishi, nimefanya tathimini nimebaini hizi fedha hazipo tena na vikundi havina uwezo tena ile hamasa haipo tena" RC Mwanza.
Sambamba na hilo ameshauri elimu hiyo kuanza kutolewa kuanzia ngazi ya shule za msingi ili kujenga jamii yenye weledi mkubwa wa masuala ya fedha.