Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msako waliotoweka na mtoto mwenye ualbino washika kasi, DC Muleba atoa maagizo

Albino Aliepoteaaaa Picha ya mtoto mwenye Ualbino, Asimwe Novath (2) ambaye ametoweka baada ya watu wawili kumpoka

Mon, 3 Jun 2024 Chanzo: Mwananchi

Siku tano tangu watu wasiyojulikana kudaiwa kumkwapua mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novath (2) na kutoweka naye kusikojulikana, Mkuu wa Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, Dk Abel Nyamahanga ameliagiza Jeshi la Polisi kumtafuta mtoto huyo kwa gharama yoyote.

Pia, amewaagiza maofisa watendaji wa vijiji kufanya sensa yenye lengo la kufuatilia na kubaini kaya zenye watu wenye ualbino wilayani humo, ili kurahisisha utambuzi na kuimarisha ulinzi na usalama wao.

Asimwe alichukuliwa na watu hao waliofika nyumbani kwao Kitongoji cha Mbale Kata ya Kamachumu wilayani Muleba mkoani humo, Alhamisi Mei 30, 2024 na mpaka sasa Jeshi la Polisi likiwashikilia watu watatu akiwemo baba mzazi wa mtoto huyo, Novath Asimwe (24) kwa mahojiano.

Akizungumza leo Jumatatu Juni 3, 2024, alipotembelea familia hiyo, Dk Nyamahanga amesema hategemei kusikia tena tukio la mtu mwenye ualbino kutekwa ama kupotea wilayani humo.

“Uchungu wa kujifungua mtoto mwenye ualbino hauna tofauti na wa kujifungua mtoto mwingine. Wote ni watoto, hivyo kinamama mtambue hakuna tofauti, sisi kama Serikali tunasema hatutolala mpaka mtoto apatikane kwa gharama zozote,” ameagiza mkuu huyo wa wilaya.

Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Yusuph Daniel amesema maofisa wa jeshi hilo wanaendelea kumtafuta mtoto huyo na watuhumiwa wengine wanaodhaniwa kuhusika katika tukio hilo.

Bila kuweka wazi, Kamanda Daniel amesema katika uchunguzi unaoendelea ni vigumu kuweka wazi iwapo tukio la kupotea kwa Asimwe (mtoto mwenye ualbino) linahusiana na imani za kishirikina.

"Hatujakamata mtuhumiwa anayekiri moja kwa moja kuhusika na mwisho wa uchunguzi wetu tutaelezea tulichokigundua," amesema Daniel huku akidokeza kuwa bado wanawashikilia watu watatu akiwemo baba wa mtoto huyo.

Akizungumza na Mwananchi Digital jana Juni 2, mwaka huu, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Watu wenye Ualbino nchini (TAS), Alfred Kapole alipendekeza iwapo Jeshi la Polisi limeshindwa kufanya msako na kumpata mtoto, jukumu hilo likabidhiwe kwa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

"Kama Jeshi la Polisi wameshindwa kabisa kuwakamata na kutokomeza matukio ya aina hii, basi waruhusu Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) waingilie kati. Haiwezekani mtu anatoka huko anamnyang'anya mtu mtoto halafu tangu Alhamisi, lakini hadi sasa hawajamkamata wala kumpata," alisema.

Kwa mujibu wa Kapole, mbali na kuwashtua, tukio hilo liliibua taharuki kwa watu wenye ualbino, jambo linaloweza kusababisha wasijiamini na kuachana na shughuli za uzalishaji mali na ujenzi wa Taifa.

"Ni Jambo la kusikitisha kwamba Tanzania ni nchi yetu sote, lakini mtoto huyu (Asimwe) tangu atekwe na watu hao hajapatikana wala watuhumiwa hawajakamatwa. Sasa tafsiri ya Tanzania ni nchi ya amani iko wapi?

"Tunaiita Tanzania kisiwa cha amani; haiwezi kuwa kisiwa cha amani kwa watu fulani wakati wengine hawana amani, ni sawa na kuwa na watoto saba, ukiwanunulia nguo, mmoja ukamuacha atajisikia vibaya. Tunakosa amani kwa jamii inayotuzunguka, ndoa zitavunjika, tumepanga katika majumba ya watu, tutafukuzwa," alisema Kapole.

Alitoa historia kuwa kuna matukio mengine ya watu wenye ualbino kushambuliwa, kunyofolewa viungo na kuuawa, lakini Jeshi la Polisi halitoi taarifa ya hatua za kisheria zinazochukuliwa kwa watuhumiwa.

Chanzo: Mwananchi