Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Saad Mtambule ametoa siku tano kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri daladala na magari binafsi yote yanayodaiwa fedha za maegesho kuhakikisha wanalipa madeni hayo.
Mtambule amebainisha hayo leo Juni 20, 2024 mara baada ya kukutana na viongozi wa madereva na wamiliki wa vyombo vya usafiri yaani daladala wa wilaya ya Kinondoni ambapo aliwataka kulipa madeni hayo ikiwa ni maelekezo kutoka kwa Waziri wa TAMISEMI, Mohammed Mchengerwa.
"Wale wote wenye madeni ya maegesho ya magari wahakikishe kwenye kipindi cha siku tano hizo pesa wawe wamelipa na katika kuhakikisha wanalipa tumepeleka vikosi kazi kwenye maeneo mbalimbali.
"Ikumbukwe deni lililoainishwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali kwa Manispaa yetu ya Kinondoni ni shilingi bilioni 2.9 hivyo ni sharti hizo pesa tuzikusanye," amesema Mtambule.