Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msacky; mlemavu mmiliki wa kampuni aliyeajiri watumishi

43584 Pic+mlemavu Msacky; mlemavu mmiliki wa kampuni aliyeajiri watumishi

Mon, 25 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Changamoto kwa wenye ulemavu hujitokeza mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ambapo licha ya elimu kutolewa baadhi ya watu wamekuwa wagumu kuelewa, kwenda na wakati.

Hussein Msacky (32) ni mmoja wa watu wenye ulemavu anayesema amepitia changamoto mbalimbali hadi kufikia alipo sasa.

Anasema akiwa ni mtoto wa nne katika familia ya watoto sita ya Mzee Msacky na mke wake Maridhia Said, wakazi wa Kata ya Bondeni, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro kama sio uimara wa wazazi wake asingekuwa hai.

Anasema amezaliwa akiwa na ulemavu wa mikono na miguu, hali iliyowafanya wataalamu wa afya katika hospitali ya KCMC alikozaliwa wasiruhusu kupelekwa nyumbani.

Hussein ambaye tayari amefunga ndoa na kumiliki kampuni ya ujenzi na kunyunyiza dawa za kuua wadudu ya Mchakamchaka Construction, anasema baada ya kuzaliwa alikaa KCMC kwa miaka saba ili kupata matibabu na huduma muhimu kutokana na hali yake.

Akizungumza na gazeti hili kuhusiana na historia ya maisha yake, anasema baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali akiwa na miaka minane, alikumbana na changamoto ya kukataliwa na jamii iliyoiwazunguuka.

“Nilipajua nyumbani kwetu nikiwa na umri wa miaka minane kutokana na kukaa hospitali kwa muda mrefu. Nashukuru ujasiri wa familia yangu ulisaidia kuniweka salama mpaka nilipofikia,” anaeleza Hussein.

Anasema kwa nyakati na mazingira tofauti amekuwa akikumbana na kauli za kuudhi ikiwamo kudaiwa kuwa kuzaliwa kwake katika familia hiyo kunaashiria ilikuwa na laana.

“Mpaka kufikia leo nimekuwa kijana ninayejitegemea, kuendesha maisha yangu na kuwasaidia wengine, nimepitia changamoto nyingi, lakini familia yangu ilitambua thamani yangu kama binadamu,” anasema.

Kwa mujibu wa Hussein, hata familia yake ilipomwandikisha darasa la kwanza ilikumbana na kebehi na dharau ikidhaniwa kuwa asingeweza kufanikiwa.

“Mama yangu alikuwa mwalimu katika Shule ya Msingi Mawenzi, alidharauliwa na jamii wakiwamo wafanyakazi wenzake kwa ajili yangu, lakini namshukuru sana kwa kuwa hakukata tamaa, aliendelea kunipenda na kunithamini,” anasema.

Anaeleza: “Nilipofika darasa la tano, mama yangu aliacha kazi ya uwalimu na kuwa mkulima, ili aweze kunihudumia kwani kutokana na hali yangu, nilihitajika uangalizi wa karibu na kila mara nilihitajika kurudishwa hospitalini”.

Mazingira ya elimu

Hussein anaeleza kuwa, alipata elimu ya Msingi katika Shule ya Msingi Mawenzi kisha alijiunga na Shule ya Sekondari Kibo, ambako alisoma kwa mwaka mmoja na baadae kuhamia shule ya sekondari Mount Kilimanjaro kutokana na mazingira ya shule ya awali kutokuwa rafiki kwake.

“Nilisoma hapo hadi kidato cha nne licha ya changamoto ya madarasa kuwa ghorofani. Baadae nilijiunga na kidato cha Tano katika Shule ya Sekondari Majengo ambako nilihitimu kidato cha Sita na kujiunga na Chuo cha Elimu ya Biasha (CBE)” anasema. Kwa mujibu wa Hussein, baada ya kuhitimu masomo ya uhasibu chuoni hapo alipata wakati mgumu kupata ajira kwani baadhi ya watu walimuona ni mzigo na kumhukumu kuwa hataweza kufanya kazi “nikafungua duka la vitabu huku nikiendelea kutafuta ajira”.

“Kabla ya kuhitimu, nilipata mazoezi ya vitendo (field), katika ofisi moja ya Serikali mkoani Kilimanjaro, na kutokana na hali yangu familia ililazimika kuajiri mtu wa kunisukuma wakati wa kwenda na nikiwa kazini ambaye alilipwa Sh.100,000 kwa mwezi,” anaeleza Hussein.

Anasema: “baadae nilipata kazi katika kampuni moja jijini Dar es Salaam, ambayo ilinilipa mshahara wa Sh300,000 kwa mwezi, kati ya hizo Sh.180,000 nilizitumia kukodi taksi kwenda kazini kwa mwezi na Sh.100,000 nilikuwa nikimlipa mtu niliyemwajiri kunisaidia”.

Walemavu wasidharauliwe

Anasema kutokana na mazingira aliyoyapitia anaamini wapo wengi wenye hali kama yake wanaoweza kutoa mchango mkubwa kwa jamii iwapo watapewa nafasi, kuungwa mkono na jamii kwa kile wanachokifanya kwa maendeleo ya nchi.



Chanzo: mwananchi.co.tz