Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mradi wachepushwa kulikwepa kaburi la mzee wa kimila

Kaburi Pic Data Mradi wachepushwa kulikwepa kaburi la mzee wa kimila

Wed, 10 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katika kuheshimu mila na desturi, Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) limelazimika kuchepusha mradi wake ili kukwepa kaburi la mmoja wa viongozi wa kimila katika Kijiji cha Gorimba wilayani Hanang.

Katika kutekeleza uchepushaji huo, EACOP imelazimika kutia saini ya makubaliano na wanajamii ya Wataturu, ambapo hafla hiyo iliyofanyika leo, Jumanne Januari 9, 2023 ulisimamiwa na Wendy Brown, Meneja Mkuu wa EACOP Tanzania na viongozi wa jamii ya Wataturu, wakishuhudiwa na wanajamii.

Mkazi wa eneo hilo Esther Dakhor, amesema kitendo hicho ni heshima kwao na kutaka uwekezaji unaofanyika maeneo mbalimbali kuheshimu mila na tamaduni.

“Tunashukuru wameliacha kaburi la mzee wetu wa kimila ambalo linasaidia katika masuala ya kimila. Nadhani kila uwekezaji unaofanywa sehemu usikiuke mila na tamaduni za eneo husika,”amesema.

Kwa upande wake Mshauri wa EACOP Makundi ya Kikabila, Dk Elifuraha Laltaika, amesisitiza dhamira ya mradi katika kupunguza athari kupitia ushirikiano wenye tija.

“Ni jambo jema mradi mkubwa kama huu kuepuka athari katika urithi muhimu wa kitamaduni wakati wowote kadri iwezekanavyo.

“Hatua hii ni sehemu ya kuonyesha kujali mila na tamaduni za jamii za Kitanzania pamoja na kuheshimu haki za binadamu, Kutokana na tathmini ya kina ya athari za haki za kibinadamu na mchakato wa utwaaji wa ardhi,”amesema na kuongeza Dk Laltaika.

Mradi huo utakaohusika na usafirishaji wa mafuta katika eneo hilo umezigusa jamii tatu tofauti ambazo ni pamoja na: Kimasai, Wadatoga (Wataturu na Wabarabaig), na jamii za Waakie.

Naye mwakilishi wa Jukwaa la Asasi zisizo za kiserikali za Wafugaji (Pingo), Nailejileji Tipap amesema hatua ya kulipisha kaburi hilo ni mfano wa kuigwa kwani utamaduni wa eneo husika umelindwa.

“Napongeza mradi huu wa EACOP kwa kulinda maslahi ya wazawa na kuheshimu na kuulinda utamaduni wa eneo hili,” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live