Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mradi wa ufuatiliaji fedha za miradi ya maji waleta tija

02a09c5fd78b887fa4704fa335ff9a3b Mradi wa ufuatiliaji fedha za miradi ya maji waleta tija

Fri, 19 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MRADI wa kujenga uwezo wa jamii na asasi za kiraia katika ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma katika miradi ya maji umetajwa kuleta matokeo chanya kwa wananchi kushiriki kulinda na kufanya miradi hiyo kuwa endelevu.

Hayo yalisemwa jana wakati wa kuwasilishwa kwa taarifa za mradi huo ambao unatekelezwa na Mtandao wa Asasi za Kiraia Mkoa wa Dodoma (Ngoneco) kwa ufadhili wa The Foundation for Civil Society.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mwakilishi wa Wakala wa Maji Vijijini (Ruwasa), Samson Njoweke alisema kabla ya mradi huo kutekelezwa wananchi walikuwa wakiona miradi ya maji ni ya serikali lakini sasa wamepata uelewa na kuiona ni mali yao na wanatakiwa kuitunza ili iwe endelevu.

Hata hivyo, alisema kisera bado kuna changamoto kutokana na baadhi ya mifumo kubadilika na wananchi hawajahusishwa kikamilifu.

“Sasa wananchi wamekuwa wakichukua hatua mbalimbali na uwazi na ufuatiliaji wa miradi umekuwa mzuri.

"Mimi ni mratibu wa vyombo vya watumiaji maji wilaya ya Bahi, zamani wenyeviti wa vijiji nilikuwa nawaona kama maadui lakini nilipogundua ushirikishwaji ni muhimu kwenye miradi ya maji sasa wananchi wamekuwa walinzi namba moja wa miundombinu ya maji," alisema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mchito, Abdul Machete alisema kamati za kufuatilia matumizi ya fedha za umma (Pets) zinafanya kazi vizuri, zimepewa uwezo na kila siku zinaongeza uwezo katika utendaji.

Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Honoratha Rwegasira alitaka matokeo chanya yaliyopatikana kutokana na utekelezaji wa mradi huo katika wilaya ya Bahi kuwa endelevu ili jamii iweze kuendelea kufaidika na miradi ya maji kwenye maeneo yao.

Akitoa tathimini ya utekelezaji wa mradi huo, Luhaga Makunja kutoka Ngonedo alisema wilaya ya Bahi ina vijiji 59 lakini mradi huo ulitekelezwa katika vijiji vinne ambavyo ni Mkakatika, Bahi Sokoni, Nguji na Mkito.

Alisema kwa sasa wananchi asilimia 70 ya wananchi wilayani humo wana uelewa wa miradi ya maji na ufuatiliaji wa miradi ya maji umeongezeka.

Alisema wakati wa utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi ziliundwa kamati za Pets za vijiji na awamu ya pili yalitolewa mafunzo ya ufuatiliaji zaidi ikiwamo wa nyaraka.

Alisema hadi kufikia mwaka jana, Bahi ilikuwa na asilimia 50 ya wananchi wanaopata maji safi na salama.

Chanzo: habarileo.co.tz