Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mradi wa maji kwa wakazi 4,000 Msamalo wazinduliwa

C1bce9cb47372d8aafa1a4ddea26ad8c.png Mradi wa maji kwa wakazi 4,000 Msamalo wazinduliwa

Thu, 17 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SHIDA ya maji kwa wakazi wa kata ya Msamalo, wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma kwa sasa itabaki kuwa historia baada ya kuzinduliwa kwa mradi wa maji utakaowanufaisha wakazi zaidi ya 4,000 pamoja na taasisi za kijamii kwenye eneo hilo.

Mradi huo wa maji umefanikishwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Water Mission Tanzania na serikali kupitia Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA).

Mradi huo unatumia nishati ya jua, ambapo maji yanavutwa kutoka kwenye kisima na kwenda kwenye kituo cha kusafisha na kutibu maji na baadaye yanapelekwa kwenye vituo 18 vilivyopo karibu na makazi ya watu.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Mkurugenzi wa Water Mission Tanzania, Benjamin Filskov alisema utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya mkakati wa shirika hilo katika kuunga mkono jitihada za serikali kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata maji safi na salama karibu na makazi yao.

Filskov alieleza kuwa lengo la mradi huo ni kuhakikisha wananchi wanakuwa na mfumo thabiti wa kupata maji safi na salama karibu na makazi yao.

Akizindua mradi huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Antony Sanga alisema kukamilika kwa mradi huo ni utekelezaji wa ahadi za serikali katika kupunguza kero ya maji kwa wananchi.

Aliwataka wakazi wa Msamalo kuendeleza mradi huo ili uwe endelevu kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Water Mission ni shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na kubuni, kujenga na kutoa miundombinu na suluhisho mbalimbali za maji pamoja na usafi (WASH) kwa nchi zinazoendelea na zinazokumbwa na majanga mbalimbali.

Water Mission imekuwa ikiendeshwa nchini Tanzania tangu mwaka 2013 na kwa mwaka huu pekee jumla ya watu 350,500 wamenufaika na miradi ya maji iliyotekelezwa nchini kwenye vijiji, maeneo ya mafuriko, kambi za wakimbizi pamoja na hospitali.

Chanzo: habarileo.co.tz