Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mradi wa maji kunufaisha Kijiji cha Chimate

0e1dbec37344b1c36548ebd1f4391635 Mradi wa maji kunufaisha Kijiji cha Chimate

Wed, 7 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI ‘imewatua ndoo’ wananchi wa Kijiji cha Chimate wilayani Nyasa katika Mkoa wa Ruvuma baada ya kutekeleza mradi wa maji uliogharimu Sh milioni 390.

Akisoma taarifa ya mradi huo, Meneja Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Wilaya ya Nyasa, Mhandisi Jeremia Maduhu alisema mradi huo umekamilika kwa zaidi ya asilimia 85 na unatekelezwa kupitia mfumo wa ‘force account’.

Alisema mradi huo utakapokamilika unatahudumia wananchi 2,798 wa Kijiji cha Chimate na kwamba, ujenzi wake ulianza Julai Mosi, 2020.

“Kazi zilizopangwa kutekeleza kwenye mradi huu ni ujenzi wa chanzo kipya cha maji, ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 75,000, ujenzi wa vituo 15 vya kuchotea maji na ujenzi wa mtandao wa bomba wenye urefu wa kilometa 15,’’ alisema Maduhu.

Hata hivyo, alisema katika mradi huo, hadi sasa zimetumika zaidi ya Sh milioni 356 katika kutekeleza mradi huu unaotarajiwa kukamilika kwa asilimia 100 kabla ya kuisha kwa mwezi huu.

Alizitaja kazi zilizokamilika kwa asilimia 100 kuwa ni ujenzi wa chanzo kipya cha maji, tanki la kuhifadhia maji na ujenzi wa vituo 18 vya kuchotea maji.

Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi katika mradi huo, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Isabela Chilumba, alisema mradi huo utaondoa kero ya maji kwa wananchi hao na kuwapongeza Ruwasa kwa kusimamia mradi huo.

Meneja wa Ruwasa katika Mkoa wa Ruvuma, Rebman Ganshonga, alitoa rai kwa wananchi wa kijiji hicho kuhakikisha wanasimamia, wanatunza na kukilinda chanzo cha maji ili mradi huo uwe endelevu.

“Wananchi wa Chimate, hiki chanzo tunachotumia kwenye mradi huu ni chanzo cha mtiririko kwa hiyo, tafadhali sana msifanye kazi za kibinadamu hapa; mkiharibu mtambue kuwa tutakuwa tumepoteza fedha za serikali na maji yatakauka,’’ alisema Ganshonga.

Akizungumza kwa niaba ya wanawake wa Kijiji cha Chimate, Mary Ndembeka, alisema kabla ya mradi huo, baadhi yao ndoa zilikuwa njia panda huku wanawake wengine wakipigwa mara kwa mara na waume zao kwa kuchelewa kutoka kuchota maji na kwamba changamoto hizo sasa zitaisha kupitia mradi huo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz