Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mradi wa maji Chalinze wamuibua naibu waziri

38322 MRADI+PIC Mradi wa maji Chalinze wamuibua naibu waziri

Fri, 25 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Pwani. Naibu waziri wa maji, Jumaa Aweso amemuagiza katibu mkuu wa wizara hiyo, Profesa Kitila Mkumbo kuitisha mkutano kujadili mradi wa maji wa Wami-Chalinze ambao unaonekana kusuasua.

Akizungumza leo, Januari 24, 2019 wakati wa ziara ya kikazi mkoani humo kwa lengo la kukagua maendeleo ya mradi huo, Aweso alisema hayupo tayari kuona mradi huo unakwama kwa sababu umegharimu fedha nyingi ambazo ni kodi za wananchi.

Jana, Rais John Magufuli alipokutana na viongozi wa dini jijini Dar es Salaam aliuzungumzia mradi huo akisema umegharimu fedha nyingi huku kukiwa hakuna maendeleo yoyote.

Mradi huo umegharimu Sh95 bilioni na ulitakiwa kukamilika Desemba mwaka jana hata hivyo hadi sasa umefikia asilimia 78.

Rais Magufuli alisema Serikali imeshalipa fedha nyingi kwa mkandarasi lakini haujaanza kutoa maji na kwamba Serikali imelazimika kushikilia pasipoti za mkandarasi ili aukamilishe.

Kauli ya Rais imemuibua naibu waziri huyo ambaye  amefika eneo la mradi na kutoa maagizo makali kwa wasimamizi wa mradi huo huku akisema ni lazima ukamilike kwa manufaa ya wananchi.

"Kikubwa kinachoonekana hapa mhandisi mkuu ni changamoto, kwa hiyo tunawasihi sana wataalamu wetu lazima watafute wakandarasi wenye uwezo na sasa kwa sababu huyu amepatikana atakuwa funzo kwa wengine," alisema Aweso.

Ameongeza "Hatuwezi kukubali fedha alizokula ashindwe kukamilisha mradi huu."

Msimamizi wa mradi kutoka Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa) Mhandisi Modesta Mushi amesema wameshalipa asilimia 62 ya fedha kwa mkandarasi na hadi sasa umefikia asilimia 78.

Kutokana na hali hiyo, Aweso alimtaka katibu mkuu wa wizara hiyo, Profesa Kitila Mkumbo kuitisha mkutano siku ya Jumanne (29, Januari) mjini Dodoma ili kutafuta ufumbuzi.

"Tunamuagiza katibu mkuu kuitisha kikao cha haraka ndani ya wiki hii ili wadau wote wanaohusika na mradi tubanane ili mradi uweze kukamilika," alisema.

Meneja Mradi wa Kampuni ya Overseas Infrastracture Alliance (OIA) PV Ltd ya nchini India inayojenga mradi huo, Rajaw George alisema pamoja na changamoto zilizopo, wanategemea kukamilisha mradi huo kulingana na makubaliano na Serikali ya Tanzania.

Naye mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Zainab Kawawa alisema changamoto ya maji ni kubwa na kwamba atahakikisha anatenga muda wake kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji.

"Sisi kazi yetu ni kuendelea kumbana mkandarasi ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa sababu wananchi wanategemea kuona wanapata huduma za maji," alisema Kawawa.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz