Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mradi wa Tehama kuwapa ujuzi wasichana wazinduliwa

A8d853a1f986ba094e712ca91ed394df Mradi wa Tehama kuwapa ujuzi wasichana wazinduliwa

Fri, 14 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MRADI mkubwa wa kuwawezesha wasichana kupata maarifa na ujuzi wa stadi za kazi kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) umezinduliwa wilayani Kilwa.

Mradi huo ni mahususi katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazomkwamisha mwanamke na mtoto wa kike kufikia malengo yake.

Mradi huo utaendeshwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya YAPO Tanzania inayojishughulisha na uwezeshaji wa makundi ya wanawake, wasichana na vijana yenye makao yake makuu jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la Elimu la Jumuiya ya Madola, Mratibu wa Azaki katika Wilaya ya Kilwa, Fredy Mpondachuma aliwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika mradi huo ili kuwapatia nafasi wanawake kujikwamua kiuchumi.

Mradi huo umelenga zaidi kuwapatia mafunzo ya ujuzi wasichana walio nje ya mfumo wa shule kama vile matumizi ya kompyuta, uzalishaji wa bidhaa kama vile sabuni za maji, kilimo cha kisasa, usindikaji na fungashaji wa vyakula, pia watapata mafunzo ya ujasiriamali, stadi za maisha, uongozi pamoja na mafunzo ya afya ya uzazi.

Akimwakilisha Mkurugenzi wa wilaya ya Kilwa, Renatus Mcharu, mratibu huyo alisisitiza wasichana na wanawake watakaoshiriki katika mradi huo kuchangamkia fursa hiyo kwa kwa sasa ulimwengu upo katika mtandao.

Alisema wanawake hao wanaweza kusonga mbele katika maendeleo endelevu kama watajifunza matumizi ya Tehama katika kusaka taarifa na kutoa taarifa zinazowahusu wao, jamii na maendeleo yao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo ya YAPO, Salim Mpanda akifafanua zaidi kuhusu mradi huo alisema kwamba umelenga kuhakikisha kwamba wanawake wanatambua haki zao na namna ya kuzishughulikia. A

lisema mathalani wanawake wanatakiwa kutumia Tehama kukabiliana na janga kama la virusi vya corona ambalo limesababisha kuongezeka kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wasichana kama vile ndoa za utotoni na mimba za mapema.

Chanzo: habarileo.co.tz