Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mradi wa Rufiji wazaa matunda

964fdf47f3beb73943eff229ee6aacc7 Mradi wa Rufiji wazaa matunda

Sun, 19 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MRADI wa Bwawa la kufua umeme wa maji la Julius Nyerere kwenye bonde la Mto Rufiji (JNHPP), unaendelea kwa kasi na matunda yake yameanza kuonekana kwa wananchi na kwa kuchangamsha uchumi wa nchi.

Mhandisi Mkazi wa mradi huo, Mushubila Kamuhabwa aliwaambia waandishi wa habari waliotembelera mradi huo juzi kwamba hatua zote nane za utekelezaji wa ujenzi, zinaendelea kwa kasi inayohitajika.

Alitaja hatua hizo ni ujenzi wa njia kubwa ya ardhini ya mchepuko wa maji, sehemu ya kufua umeme, ukuta utakaotengeneza bwawa, eneo la kupokelea umeme unapozalishwa, barabara na madaraja, na kuchakata mawe yanayotumika kutengeneza zege na mahitaji mengine.

Alisema mradi huo utakaozalisha Megawati 2115, una miradi mingi ndani yake na yote iko katika hatua mbalimbali, huku mafundi wakiwa kazini wakiendelea na ujenzi kwa kasi.

Akizungumzia kuanza kwa manufaa ya mradi, Kamuhabwa alisema, “Jambo la kufurahisha ni kwamba tayari mradi umeanza kuchangamsha uchumi wa nchi.” Alitoa mfano kuwa wakati wakiweka zege kwenye njia ya kuchepusha maji, zaidi ya tani 200 za nondo zimetumika, hatua inayonufisha viwanda nchini.

Manufaa mengine yaliyoanza kuonekana kwa wananchi wanaoishi kwenye vijiji vinavyozunguka eneo la mradi ni upatikanaji wa miundombinu wezeshi kama vile umeme unaotoka Morogoro kupitia kwenye vijiji kadhaa.

“Lingine ni zaidi ya vijana wa Kitanzania wapatao 4,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini, hususan yale yanayozunguka eneo la mradi, wameajiriwa na wanashiriki katika mradi kwa ari kubwa,” alisema Kamuhabwa.

Kwa mujibu wa mhandisi huyo, wanatarajia idadi ya ajira itaongezeka kufikia watu 6,000 mradi utakapofikia hatua ya juu zaidi. Baadhi ya wanakijiji cha Kisaki, kilichopo kilometa 60 kutoka kwenye mradi, walimpongeza Rais John Magufuli kuanzishwa kwa mradi huo. Walikiri kuanza kuona manufaa yake, ikiwa ni pamoja na ukuaji wa biashara.

“Kisaki inakuja juu, tuna uhakika mradi ukimalizika Kisaki itakuwa kama Morogoro. Kwa sasa biashara inakua kwa kasi sana tofauti na hapo awali. Kwa mfano, mchele tunauza kilo kwa shilingi 1,600 tofauti na hapo awali tulikuwa tunauza shilingi 500. Bei ya juu ilikuwa shilingi 1,000. Watu wameongezeka sana,” alisema Ali Matumbo.

Matumbo alikiri kijiji hicho kufikiwa na umeme, ambao umenufaisha wananchi wengi ikiwamo shule iliyopata nishati hiyo. Mwanakijiji mwingine, Asha Said alieleza kufurahishwa na wageni wengi wanaofika katika kijiji hicho cha Kisaki na kuchangamsha biashara zao.

Alisema ana matumaini, watapata barabara nzuri kutokana na mradi huo. Hassan Ngozi aliwaambia waandishi wa habari kwamba anayo matumaini makubwa, kwamba mradi utakapokamilika, watakuwa na Kisaki mpya.

“Kwetu sisi ongezeko la watu hapa Kisaki limekuwa na faida kubwa...watu wakienda kufanya kazi huko kwenye mradi, wanakuja hapa kijijini wananunua bidhaa zetu na sisi tunapata pesa, haya ni manufaa makubwa kwetu,” alisema

Chanzo: habarileo.co.tz